Wajionaje na hali? Familia yako kwa ujumla haijambo? Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu. Napata haki yangu kupitia taaluma yangu na maisha yanazidi kuyoyoma.
Madhumuni ya kukuandikia barua hii ni kutaka kukueleza kwamba sikufurahishwa sana na mgogoro ulioendeshwa na wake zako ambao kimsingi niliamini ulikuwa unaweza kuepukika kabla ya kuwafaidisha watu.
Wiki iliyopita haikuwa nzuri sana kwako. Kwa kuwa Watanzania wanakuheshimu, wanakuamini naamini hawakufurahishwa na malumbano yaliyoibuliwa na wake zako. Naamini hata wewe hayakukufurahisha. Ndoa yako imejadiliwa sana mitandaoni.
Mmewapa sana nafasi watu kuzungumza vitu ambavyo havikuwa na sababu ya kuzungumzwa.
Kutukanana, kushutumiana mambo mazitomazito halikuwa jambo jema. Ilileta picha mbaya kwa mashabiki wako na wale wa Jahazi. Kama baba, ulipaswa kulidhibiti kabla halijatoka nje.
Nasema hivyo kwa sababu vitu ambavyo walianza kuvizungumza vilikuwa ni vya kujidhalilisha wao wenyewe na wewe pia.
Kwa kuwa wote ni wake zako, ulikuwa na nafasi ya kuwakanya wasitoe siri za ndani. Kuwaambia wote wasizungumze na vyombo vya habari maana kufanya hivyo kulilifanya sakata hilo kuzidi kuwa kubwa.
Badala yake ugomvi ulikuwa mkubwa. Watangazaji nao wakadandia sakata hilo. Kila mmoja akawa na upande wake, mwisho wa siku ilikuwa ni fedheha kwa familia yako.
Sakata hilo limewafanya hata ambao hawakuwa na wazo la kujadili maisha yenu binafsi, kuanza kufanya hivyo. Nakushauri kama bado hujaamua, amua sasa. Kaa nao chini na kubaini kiini cha ugomvi. Kujua nani alianza na nini ufanye ili uweze kumaliza tofauti.
Wanawake ni mama zetu, lakini tunafahamu mara nyingi huwa ni rahisi kukuza ugomvi mdogo na kuufanya uwe mkubwa. Pengine chanzo kilikuwa ni kidogo, waeleze ukweli kwamba hawapaswi kuyatoa nje mambo yao.
Waeleze kwamba madhara ya hivyo ni kujidhalilisha na kuwafanya waonekane hawajafundishwa na wazazi wao. Waeleze kwamba wewe ni nani, una heshima gani katika jamii, hivyo waishi kulingana na heshima yako. Waache mambo yale ya ‘kiswahili’.
Ikiwa unaona unazungumza kama mume na bado mmoja wao au wote wanakuwa hawakuelewi, ni vyema kuchukua hatua kali zaidi. Heshima yako umeijenga kwa muda mrefu, ni vyema kushirikisha hata wazazi kusaidia kutatua mgogoro huo.
Simama kama mwanaume. Kuwa mkali pale inapobidi kufanya hivyo maana wakati mwingine wapo baadhi ya wanawake wanaojaribu kutikisa kiberiti ili waone ndani kina nini. Ukiwa mkali, utamuona amenywea.
Nakuamini maana ni muda mrefu uliweza kudhibiti mikwaruzano ya kifamilia kutoka nje. Naamini katika hili imepenya bahati mbaya. Unajua wapi imepenyea, basi jitahidi kudhibiti isitokee tena siku za usoni.
Ni matumaini yangu utasimama kama mwanaume na mgogoro huo utaisha na hata siku nyingine hatutasikia mambo binafsi yanatoka katika vyombo vya habari.
Mimi nduguyo;
Erick Evarist
Global PublishersWEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment