Meneja Uhusiano wa NHC, Yahya Charahani amelieleza Gazeti la Nipashe kuwa, walimpatia notisi Askofu Gwajima ya kuhama eneo hilo mwezi mmoja uliopita, lakini hakutekeleza badala yake ameendelea kulitumia eneo hilo kuendesha shughuli za kanisa lake, zikiwamo ibada.
Charahani alisema eneo hilo ni mali ya NHC na ni maalum kwa ajili ya ujenzi wa mji wa kisasa na wakazi waliokuwa wanaishi eneo hilo walishalipwa fidia muda mrefu uliopita ili kuondoka.
“Lile eneo ni la NHC kwa muda mrefu na kabla ya hapo kulikuwa na nyumba nyingi sana na zilibomolewa, hizo zilizobaki zimebaki tu kimakosa,” alisema Charahani.
Aliongeza kuwa, hiyo siyo mara ya kwanza kwa NHC kumpatia notisi Askofu kiongozi huyo kulihamisha kanisa lake.
Kwa mujibu wa Charahani, NHC walimpatia notisi Askofu Gwajima ya mwezi mmoja kuondoka katika makazi hayo na kwamba notisi hiyo ilimalizika Machi 9, mwaka huu.
Alisema baada ya kumalizika kwa notisi hiyo, NHC lilimpatia muda zaidi Askofu huyo ambao unamalizika leo.
Juhusi za kumpata Askofu Gwajima kuthibitisha kama amepokea notisi hiyo zilishindikana kutoka na simu yake ya mkononi kutopatikana kila alipopigiwa tangu Alhamisi iliyopita.
Hata hivyo, jana alipotafutwa Mwanasheria wa Askofu Gwajima, Paul Mallya kuelezea hatua ya NHC ya kumpa mteja wake notisi ya kuhamisha makao ya kanisa lake, alisema bado hajapata notisi hiyo.
“Sijapata taarifa hiyo, ndiyo kwanza nasikia kwako, ngoja nifuatilie nije nikupe majibu yaliyokamilika,” alisema Mallya. WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment