WATU wawili akiwemo jambazi mmoja na
askari mwanafunzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamekufa na wengine
kunusurika kuuawa katika tukio lililotokea juzi, mjini Mafinga mkoani
Iringa wakati majambazi wakirushiana risasi na askari wa Jeshi la
Polisi.
Risasi hizo zilipigwa wakati Polisi hao
wakijaribu kuokoa fedha za mfanyabiashara Salama Semwaiko zilizoporwa na
majambazi wawili waliotumia pikipiki wakati wakifanya uporaji huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
Ramadhani Mungi alisema mfanyabiashara huyo aliporwa fedha hizo juzi
majira ya saa 2.45 asubuhi alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda
kwenye biashara zake.
Tukio hilo la kusikitisha lililovuta
hisia za watu wengi na kufanya baadhi kuzimia wengine kukimbia hovyo na
kujifungia ndani kwa ajili ya kuokoa maisha yao lilitokea katika eneo la
Kinyanambo B, nje kidogo ya mji wa Mafinga.
Kamanda Mungi alisema; “mfanyabiashara
huyo akiwa katika gari lake akielekea kwenye biashara zake mjini
Mafinga, mfanyabiashara huyo alisimamishwa na mtu mmoja aliyekuwa amevaa
koti jeusi na baada ya kusimama alimtolea silaha na kumtaka atoe fedha
na vitu vyote vya thamani alivyokuwa navyo .”
“Baada ya kuona hana msaada
mfanyabiashara huyo alijikuta akilazimika kutoa Sh 700,000 alizokuwa
nazo, simu ya mkononi na baadaye ilitokea pikipiki ambayo haikufahamika
namba za usajili na kumpakia mtu huyo na kuanza kukimbilia eneo la
Kinyanambo,” alisema.
Alisema mara baada ya majambazi hao
kutoweka, Jeshi la Polisi lilipewa taarifa na kuwahi eneo la tukio na
kwa kushirikiana na wananchi walianza kuwakimbiza majambazi hao na ndipo
majibizano ya risasi yalipoanza.
Katika hekaheka hiyo, Kamanda Mungi
alisema Said Ngudi (25) ambaye ni askari wa JKT Makutupora, Dodoma
alipigwa risasi na kufa papo hapo wakati akisaidia kupambana na
majambazi hao.

0 comments:
Post a Comment