Ofisi ya Bunge imesema haijapata barua yoyote kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Kauli ya hiyo ya Bunge imekuja siku moja baada ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza kumvua uanachama Zitto,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema kutokana na hali
hiyo, Zitto bado ni mbunge halali wa Kigoma Kaskazini na kwamba
anapaswa kuendelea na shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Dk Thomas Kashililah, amebainisha kuwa endapo Bunge
litapata taarifa rasmi ya Chadema kumvua uanachama Zitto, lazima Bunge
hilo lifanye kwanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo litoe
uamuzi.
Pia amesema sakata la mbunge wa Bunge hilo kuvuliwa
uanachama na chama chake si la kwanza, kwani tayari kuna mbunge
aliyevuliwa uanachama na chama chake lakini Bunge hilo halikumvua
uanachama wake baada ya kumaliza uchunguzi wake. Hata hivyo hakumtaja
mbunge huyo.
“Utaratibu ulivyo, chama huliandikia Bunge kuhusu kumvua
uanachama mbunge na Bunge kabla ya uamuzi wowote hufuatilia kwanza
sababu za kuvuliwa uanachama huo, ili kujiridhisha kama zilikuwa halali
au la,” alisema Kashililah.
Alisema baada ya hapo Bunge hilo huwasiliana na Msajili wa
Vyama vya Siasa ili ofisi hiyo ya msajili iweze kupitia Katiba ya chama
husika na kupitia sababu za chama husika zinazoweza kumvua uanachama
mwanachama wake na kama kweli zimekiukwa.
“Baada ya suala hilo kupelekwa kwa msajili wa vyama vya
siasa, Spika wa Bunge, hutoa uamuzi baada ya kuchunguza na uamuzi huo,
hupelekwa kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa ajili ya kufanyiwa
kazi zaidi,”alisisitiza.
Aidha alisisitiza: “Si lazima Spika akubaliane na uamuzi
wa kutengua ubunge wa mbunge husika kwani kama haikuwa halali kwa
mbunge huyo kuvuliwa uanachama, Spika hubatilisha uamuzi wake wa kumvua
ubunge mhusika,” alisema.
Alisema Spika Anne Makinda katika kipindi chake alishawahi
kutoa uamuzi wa kubatilisha mbunge fulani kuvuliwa ubunge hata baada ya
chama chake kumvua uanachama.
Akizungumzia suala hilo, Zitto, alisema kwa upande wake
bado ni mbunge na anaendelea na kazi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) hadi pale atakapopatiwa taarifa rasmi
ya kuvuliwa uanachama na ubunge wake.
“Naendelea na kazi kama vile hakuna kilichotokea, sina
taarifa yoyote ya kuvuliwa uanachama wangu wala ubunge, habari hizi
nimezisikia kwenye vyombo vya habari, sijaitwa na Mahakama kuambiwa
kinachoendelea,”alisema Zitto.
Alisema kwa sasa anaendelea kuongoza kamati hiyo na jana
alikutana na menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), leo
kamati yake inatarajia kukutana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pia
watakutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu
kuhusu mapato ya akaunti za madini.
Aidha alisema pamoja na kuendelea kama kawaida na shughuli
zake za kibunge bungeni, pia anatarajia kesho kwenda Kigoma kwa ajili ya
shughuli za maendeleo jimboni kwake, kabla ya kuhudhuria vikao vya
Bunge vinavyotarajiwa kuanza rasmi Machi 17, mwaka huu.
Alisema kwa upande wake, anachukulia suala hilo kama
changamoto ambayo inazidi kumkuza na kumkomaza katika medani za siasa
nchini na duniani kote.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene
alisema chama hicho kinajitahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa
kuzingatia sheria na taratibu zote, ikiwemo kuandaa na kuiwasilisha
wakati wowote barua inayomvua uanachama Zitto, ili suala hilo lifanyiwe
uamuzi mapema.
“Kwa sasa suala hili la Zitto limewaingia Watanzania
wengi, sasa sisi tunataka tulifanyie kazi mapema, ili uamuzi ufanywe
mapema na suala hili liishe. Kuna mambo mengi ya maana yanahitaji
kujadiliwa kitaifa kama vile masuala ya uandikishaji katika Daftari la
Wapiga kura kwa mfumo wa BVR,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye juzi
alitangaza kuwa chama hicho kimemvua uanachama mbunge huyo, jana
alimwambia mwandishi kuwa, jopo la wanasheria wa chama hicho
litaifikisha taarifa ya Zitto kuvuliwa uanachama kwa Kamati Kuu ya
chama ifikapo Mei, mwaka huu.
Alisema, "Kutokana na utaratibu uliopangwa wa Kamati Kuu
kukutana kila baada ya miezi mitatu, suala la Zitto litasubiri kikao
kingine cha kawaida cha kamati hiyo kitakachokaa mwezi Mei. Kikao
kilichopita kilikaa Februari mwaka huu".
Kwa maelezo ya Lissu, baada ya hapo ndipo wataiandikia
barua Tume ya Uchaguzi (NEC) kuijulisha kuwa Zitto si mwanachama wa
chama hicho tena au la.
You might also like:
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment