DADA wa msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Seleman Msindi ‘Afande Sele’ Zaria Kambi (30) ambaye alikuwa ni mhudumu wa baa, amekutwa ameuawa kikatili katika Gesti ya Stavi (Gesti ya Marafiki) iliyopo Kichangani, mjini Morogoro.
Tukio hilo la kinyama lilitokea usiku wa Jumapili iliyopita baada ya marehemu kuwa amekubaliana kulala pamoja na mteja aliyekuwa akimhudumia kinywaji, ambaye pia alikuwa amechukua chumba katika nyumba hiyo hiyo iliyokuwa na baa.
Kwa mujibu wa rafiki wa marehemu, ambaye pia alikuwa ni mhudumu wa gesti hiyo, Rehema Saleh, alisema mtu mmoja asiyefahamika, alifika kazini kwao na kupanga chumba namba 8A na baadaye alienda upande wa baa kunywa pombe akihudumiwa na Zaria.
“Mimi na Zaria (pichani) tunaishi jirani, sasa baada ya kumhudumia na yeye kununuliwa pombe, wakakubaliana walale pamoja, tunaishi jirani hivyo kila siku baa ikifungwa tunaongozana na jana tuliongozana njiani aliniambia amepata kichwa hivyo anakwenda nyumbani kuaga na baadaye arejee kwa bwa’nake huyo ambaye ni mara ya kwanza anaonana naye,” alisema Rehema na kuongeza.“Cha ajabu saa 8 usiku napigiwa simu na mlinzi akidai Zaria amenyongwa na mteja wake, sikuwa na jinsi, kulipokucha nilifika hapa gesti na kukuta mwili wa marehemu ukiwa kitandani,” alisema na kuangua kilio.
Mlinzi wa gesti hiyo, John Emmanuel akizungumzia tukio hilo, alisema majira ya saa 6 usiku Zaria aliingia katika chumba namba 8A na saa moja baadaye, akasikia kelele zikitoka chumbani humo, ambazo alihisi ni za kimapenzi.
“Sijakaa vizuri saa 8 usiku jamaa alitoka na begi lake akitaka nimfungulie aondoke huku mkononi akiwa na tiketi ya basi kuelekea Mbeya, nikamwambia kwanza twende chumbani kwake nikachunguze ndipo nimruhusu atoke, awali aligoma na mimi nikagoma kumfungulia geti, tukaganda kama dakika mbili akakubali kwenda chumbani tulipofika tukamkuta Zaria amekufa huku akiwa mtupu, nikamjulisha bosi Pascal Mafikiri ambaye aliita polisi wakamchukua mtuhumiwa na mwili wa Zaria,” alisema.
Mama mzazi wa marehemu, Mwajuma Hassani Kambi ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mwande Kata ya Kichangani kwa tiketi ya Chadema alipokea taarifa za kifo cha mwanaye Jumapili usiku.
Alisema mwanaye ameacha mtoto anayeitwa Rashid lsmail Kaliembe ambaye anasumbuliwa na uvimbe tumboni na kwamba kila mwezi alikuwa akipelekwa Muhimbili kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa, Erick Bruno, ambaye ni mkazi wa Manzese Tip Top Dar es Salaam, anashikiliwa. Marehemu huyo alizikwa Jumanne iliyopita mjini Morogoro WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment