Taasisi 1,200 duniani zitampa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya
Chadema, Edward Lowassa Tuzo ya Amani kutokana na utulivu aliouonyesha
kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza kutoka Bukavu, DR Congo, mwenyekiti wa Kamati ya Maadili,
Amani na Haki za Binadamu kwa jamii, Mchungaji William Mwamalanga
alisema Lowassa amechaguliwa jana mjini Bukavu na wajumbe 1,400 wa
mkutano huo.
Mwamalanga alisema wajumbe wanaohudhuria kongamano la amani wanatoka
mataifa ya Ulaya, Marekani, Asia na Afrika kwa kuwashindanisha wanasiasa
1,000 ili kumpata Kiongozi Bora wa Amani mwaka 2015, ambaye anajali na
kuangalia maslahi ya jamii badala ya madaraka.
Hatua ya kumpatia tuzo Lowassa ni baada ya kuelezwa kuwa amedumisha
amani hiyo hata baada ya kushindwa uchaguzi Mkuu wa Rais Oktoba 25.
Katika uchaguzi uliopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)ilimtangaza Dk
John Magufuli kuwa mshindi kwa kupata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia
58.46 wakati Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya
kura zote.
Mchungaji Mwamalanga alisema katika kongamano hilo, wajumbe walijadili
hali ya amani duniani na mchango wa wanasiasa katika kulinda amani hiyo.
Alisema kuwa wanasiasa barani Afrika wamekuwa vyanzo vya migogoro na
mauaji ya raia wakati wa uchaguzi, kama ilivyo nchini Burundi. Hata
hivyo, alisema kuwa wajumbe walipongeza ushindi wa Dk Magufuli, lakini
wakasema umetiwa dosari na hali ya kisiasa Zanzibar baada ya matokeo
kufutwa.
Alisema wajumbe wa kongamano hilo linaloshirikisha maaskofu, masheikh na
vijana kutoka madhehebu mbalimbali ya dini barani Afrika, wamemuhimiza
Rais Magufuli kumaliza utata wa uchaguzi wa Zanzibar.
Baada ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Chadema, Lowassa
alitangaza kuwa angefanya kampeni kistaarabu na kwa amani na baada ya
matokeo aliwatuliza wafuasi wa chama hicho, akisema “hakuna anayeweza
kuizuia bahati ya mtu” kwa hiyo kama amepangiwa kuwa rais, atakuwa.
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne,
aliongeza upinzani kwenye uchaguzi wa mwaka huu baada ya kuihama CCM na
kujiunga na Chadema iliyoukuwa na nguvu ya vyama vingine vitatu vya NLD,
CUF na NCCR-Mageuzi.
Kama alivyoahidi, Lowassa hakutumia mikutano yake ya kampeni kushambulia
mambo binafsi ya wagombea wengine, bali muda mfupi kuomba kura.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment