Nina ushauri kwa wana CCM wenzangu; Lowasa kuhamia CHADEMA msipaniki. Kama kweli tulimaanisha kuwa hafai, ana uchu wa madaraka, alikiuka kanuni na maadili ya chama, ni mwizi na tena ni fisadi basi inabidi tushangilie kuondoka kwake, kwani kuvuja kwa pakacha sio ndio nafuu ya mchukuzi? Ila kama tulimkata kwa maslahi ya watu wachache na ikiwa tulitumia akili ndogo kulikata jina lake basi itabidi tujilaumu wenyewe kwa lolote tusilolitarajia litakalotokea. Na tukiendelea kutumia akili ndogo za kudhani tutashinda kwa "magoli ya mikono", basi tunakwenda na maji mchana kweupe! Tukijidanganya kuwa matusi, kejeli, mipasho, maneno ya kwenye kanga na nyimbo za Komba kwamba zitabadilisha huu upepo, pia tutajikuta tunakuwa chama cha upinzani bila hata kujiandaa kisaikolojia. Mwana CCM utakuwa unajichanganya kuushambulia uamuzi wa Lowasa kuhamia CHADEMA kwa sababu kimsingi CCM yetu ilishabariki vijana kadhaa wamshambulie majukwaani ili aonekane hafai na hao vijana wakazawadiwa vyeo. Mtu tuliemuona hafai kwetu inatuuma nini akiondoka kwetu? Ukioa mke kisha ukamtuhumu mbele za watu kuwa ni mzinzi na mshirikina; kisha mkaachana na akaolewa na mume mwingine, unaanzaje kuhangaika nae tena huko alikoenda? Tuwaache wapiga kura waamue kama ni sisi CCM ama UKAWA. Hata Mh. Mwenyekiti JK alishasema kila mtu ana haki kuongoza hii nchi; tunategemea kushinda lakini haitakuwa ajabu UKAWA wakitwaa madaraka kutokana na makosa yetu kimkakati. Wana CCM tusipaniki, kukomaa kisiasa ni pamoja na kuhimili na kukubali usichotarajia!
Wenu,
Mfurukutwa wa Shina. WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment