Taarifa kutoka kwenye kikao cha Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF kilichofanyika leo, imesema kwamba Simba SC walishindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vya Mkataba, hivyo wanapoteza haki za kummiliki mchezaji huyo.
Chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa, Kamati hiyo imejiridhisha Messi hakuwahi kupewa nyuma ya kuishi na Simba SC jambo ambalo ni kinyume cha Mkataba baina yake na klabu hiyo.
Simba SC iliwakilishwa na Mwenyekiti wake wa Kamati yake ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi alifika na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kisoky.
Maamuzi haya ni faraja kwa Messi ambaye anahusishwa kwa kiasi kikubwa na kuhamia Azam FC. Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake. Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
Lakini Simba SC imeendelea kusistiza mchezaji huyo alikuwa ana Mkataba wa miaka mitatu. Awali, Sekretarieti ya TFF, chini ya Katibu wake, Selestine Mwesigwa ilizikutanisha pande zote mbili, mchezaji na Simba SC na kuamuru waketi chini na kutayarisha Mkataba mpya baada ya kuona huu wa sasa una mushkeli. Hata hivyo, Messi akakataa na kuamua kulihamishaia suala hilo Kamati ya Sheria ambayo leo imempa kile alichotaka ‘kuwa mchezaji huru’.
Safari FIFA?; Hans Poppe amesema kwamba watakwenda mbele kusaka haki zao
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Hans Poppe amesema kuwa, baada ya matokeo hayo, wanakwenda kukutana ili kujua hatua zaidi za kuchukua, lakini dhahiri hawataishia hapo.
“Tuliwasilisha ushahidi wote mbele ya Kamati, tumeonyesha mshahara wake ulikuwa kiasi gani na tumeonyesha kwa nini alikuwa anapewa laki moja (100,000) zaidi.
Ili akalipie kodi ya nyumba, lakini bado hatukueleweka. Tunaamini hapa si mwisho, vipo vyombo vingine ambavyo vitatupa haki yetu, tunakwenda kukutana kuangalia uwezekano wa kulipeleka suala hili huko,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment