Jeshi la Polisi limethibisha kupokea tuhuma za ubakaji dhidi ya mume wa
mwimbaji wa injili Flora Mbasha anayefahamika kwa jina la Emmanuel
Mbasha.
Akiongea na Tovuti ya Times Fm, kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi wa
Ilala, Marietha Minangi ameeleza kuwa jeshi hilo limepokea tuhuma hizo
kutoka kwa mlalamikaji ambaye ni binti mwenye umri wa miaka 17 na kwamba
binti huyo alifika katika kituo cha polisi akiwa na ndugu zake.
“Taarifa zimepokelewa na zinachunguzwa. Taarifa zilizokuja ni za kubaka
sasa tunazichunguza tufike mwisho tujue ni nini.” Kamanda Minangi
ameimbia tovuti ya Times Fm.
Ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mlalamikaji polisi
walienda nyumbani kwake ambapo hawakumkuta yeye na mkewe na kwamba hadi
sasa hawajapatikana.
Tovuti ya Times Fm ilitaka kupata ufafanuzi kuhusu uhusiano uliopo kati
ya mlalamikaji na mtuhumiwa kwani taarifa za awali zinadai kuwa ni
shemeji wa mtuhumiwa.
“Hayo yote yanachunguzwa, mimi siwezi kusema ni shemeji yake kabla
hatujafikia mwisho wa uchunguzi. Tutakapofikia mwisho wa uchunguzi ndipo
tutakapoweza kusema wana mahusiano gani.” Kamanda Minangi ameeleza.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment