NYUMBA
za kulala wageni katika Jiji la Arusha na viunga vyake zimeanza
kufurika kutokana na makundi ya watu yanayowasili jijini hapa kushuhudia
mwanzo wa ‘Safari ya Matumaini’ ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa
Monduli Edward Lowasa, anayoianza rasmi leo.
Mwanasiasa
huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa makada wa CCM walioonyesha
nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho anatarajiwa
kutangaza nia leo kuanzia saa 8 mchana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abed
Kaluta Jijini hapa.
Mpekuzi
imeshuhudia pilikapilika katikati ya Jiji, Mitaa ya Kaloleni, Makao
mapya, Levolosi na maeneo ya pembezoni ambako kuna nyumba za kulala
wageni, baadhi ya watu wakiulizia vyumba ambapo katika nyumba nyingi
kuna kibao kinachosomeka ‘vyumba vimejaa’.
Baadhi
ya wageni hao ambao walizungumza na Mpekuzi kwa sharti la kutotaja
majina yao walisema pamoja na kukosa vyumba wako tayari kulala nje hadi
watakapoianza ‘safari ya matumaini’ pamoja na Lowassa.
“Kukosa
vyumba si tatizo kwetu, tutalala hata uwanjani,tumesubiri sana siku hii
ambayo Mzee (Lowassa) alianza kuitaja tangu Mwaka 2013, tunamshukuru
Mungu imefika na tutaanza safari ya matumaini pamoja naye,” alisema mmoja wa wageni hao.
Kujaa huko kwa nyumba za kulala wageni, hoteli baadhi ya watu usiku wa kuamkia jana na leo walilazimika kulala kwenye magari.
Taarifa
kutoka kambi ya Lowassa zinaeleza kuwa, watu wengi kutoka kada
mbalimbali, wanatarajia kushiriki mkutano huo ambao Waziri Mkuu huyo wa
zamani pamoja na mambo mengine atautumia kueleza matarajio yake endapo
chama chake kitamteua kugombea urais.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo miongoni mwa waliokwisha wasili jijini humo ni
pamoja na Wajumbe wa NEC wa chama hicho wapatao 187 huku wengine 93
wakitarajia kuwasili usiku wa kuamkia leo.
Taarifa
hizo zinaeleza kuwa mbali na wajumbe hao pia wenyeviti wa mikoa 23
nchini nao watakuwepo leo katika uwanja huo wa Amri Abeid Kaluta.
Zaidi
wazee maarufu akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Pancras Ndejembi, Kanali
Mwisongo, na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Mirisho Sarakikya nao pia
wanatajwa kushiriki tukio la leo.
Mbali
na kufurika kwa wageni katika Jiji la Arusha wanaosubiri kwa hamu
hotuba itakayotolewa na Lowassa hii leo, pia mavazi ikiwamo sare za CCM
zenye utambulisho maalumu kwa ajili ya siku hiyo nazo zimepanda bei
mara dufu.
Wajasiriamali
wanaouza fulana zenye picha na maandishi yanayomtaja Lowassa ambazo
zilikuwa zikiuzwa kati ya sh.10,000 na 15,000 sasa zinauzwa kwa kati ya
Sh.20,000 na 25,000 hata hivyo pamoja na kupandishwa bei bado zimekuwa
adimu.
“Fulana
hii shingo ya mduara ni Sh. 20,000 na hii ya shingo ya v (form six)
nauza Sh.25,000 kaka karibu na zimebaki chache sana mpaka tuagize
zingine shughuli itakuwa imeshafanyika bora uchukue hii,”alisema mmoja wa wajasiriamali aliyekuwa ametandaza nguo hizo na sare za Chama katika moja ya mitaa jijini hapa.
Mbali
na kukamilika kwa maandalizi yote ya hotuba muhimu inayosubiriwa kwa
hamu na Watanzania ya ‘Safari ya matumaini’ kumekuwa na shamra shamra
kila kona ambapo kila mtaa watu wamekaa vikundi wakijadili kwa heri na
wengine kwa shari ‘Safari hiyo ya Matumini’.
Hali ya Uwanja
Maandalizi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa yalianza tangu juzi mapema asubuhi.
Tofauti
na miaka yote pengine tangu uwanja huo ujengwe unaweza kuwa haujawahi
kupambwa kama ambavyo ulianza kupambwa jana ambapo kazi hiyo ilitarajiwa
kukamilika saa 8. mchana jana.
Baadhi
ya mapambo yaliyokuwa na rangi za Chama cha Mapinduzi (CCM),
yalionekana kutawala zaidi katika viwanja hivyo huku mahema kwa ajili ya
tahadhari ya mvua na jua yakiwa yamefungwa.
Mbali
na mahema hayo pia magari makubwa ya mizigo yalikuwa yakipishana
kuingiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo ya upambaji lakini pia
tayari kwa shughuli nzima ya kesho.
Vyombo vya Habari
Mkutano
huo wa kutangaza nia wa Lowassa kama ambavyo umekuwa ukitangazwa kwenye
vyombo mbalimbali vya habari unatarajiwa kurushwa moja kwa moja pia na
vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.
Baadhi
ya vyombo vya habari kutoka ndani ambavyo vitarusha moja kwa moja
mkutano huo ni pamoja na Televisheni ya ITV,Channel Ten, Clouds TV,
EATV, ambapo kwa upande wa redio ni Clouds FM, Magic FM,na East Africa
Redio.
Lakini pia vyombo vya habari kutoka nchini Kenya navyo vipo Mkoani Arusha tayari kwa kufuatilia mkutano huo.
Vyombo hivyo ni pamoja na Televicheni ya Citizen, Nation na gazeti la The Standard.
Kuanza
kwa Safari hiyo ya Matumaini ya Lowassa, kumekuja baada ya kukamilika
kwa adhabu aliyopewa sambamba na makada wenzake ndani ya chama baada ya
kudaiwa kuanza kampeni na ushashawishi kabla ya wakati.
Makada
waliokuwa wamepewa adhabu na CCM mbali na Lowassa alikuwemo pia, Benard
Membe, Steven Wassira, William Ngeleja, January Makamba na Frederick
Sumaye.
Tayari
vikao vya juu vya CCM vimekwisha toa ratiba kamili ya uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, Mwaka huu ambapo kwa upande wa urais
zoezi la uchukuaji fomu kwa ngazi ya urais litaanza Juni 2 mwaka huu.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment