· Upotevu wa shilingi trilioni 1.151 Serikali kuu pekee hauvumiliki.
· Makusanyo yote yaliyotokana na kuongezeka kwa kodi 2013/14 yameyeyuka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ufisadi wa kutisha uliofanyika kwenye matumizi ya fedha za umma kama ilivyobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2013/2014 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Wakati chama kinaendelea kuzifanyia uchambuzi wa kina ripoti zote tano ili kuweka hadharani ubadhirifu mkubwa ambao mwingi hujificha kwenye maelezo ya kitaalam, tunapenda kutoa taarifa ya awali kama ifuatavyo;
· Wizara tatu , Trilioni 1.151 zimepotea
Katika uchambuzi wetu wa awali tumebaini kuwa kwa upande wa serikali kuu pekee zaidi ya shilingi trilioni 1.151 zimepotea au kuliwa na wajanja walioko serikalini , kiwangio hiki ni sawa na asilimia 5.231 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2015/16 inayoendelea kujadiliwa huko Bungeni Dodoma
Ripoti ya CAG iliyotolewa jana inaonyesha kuwa katika Serikali Kuu, Wizara tatu tu ambazo tumezifanyia Uchambuzi mpaka sasa zimepotea kiasi cha shilingi 1.151 Trilioni , wizara hizo ni;
i. Wizara ya Fedha (TRA) , Fedha zilizopotea kutokana na bidhaa ambazo zilipaswa kuuzwa nje ya Nchi ila kutokana na uzembe zikauzwa ndani ya nchi bila kulipiwa kodi zilikuwa jumla ya shilingi 836 Bilioni.
ii. Ofisi ya Waziri Mkuu , kitengo kimoja cha maafa zilipotea jumla ya shilingi 163 Bilioni.
iii. Wizara ya Ujenzi , ziliibwa jumla ya shilingi 252 Bilioni.
· Bajeti ya mwaka 2013/14 Mapato yote ya ongezeko la kodi yameyeyuka:
Mwaka 2013/14 yalifanyika maboresho ya sheria mbalimbali za kodi wakati wa Bunge la bajeti kodi ambazo kimsingi zilimwongezea mwananchi mzigo mzito wa kulipia kodi hizo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali na ili kuiwezesha serikali kuwahudumia wananchi wake .
Pamoja na ongezeko hilo la kodi ,ukweli mchungu ni kuwa fedha yote iliyokusanywa kutokana na ongezeko la kodi mbalimbali katika mwaka wa fedha 2013/14 imepotea yote katika wizara tatu tu za serikali kutokana na vitendo vya kifisadi, na hii ni kwa mujibu wa taarifa CAG .
Kodi zilizorekebishwa na mapato yake ni kama ifuatavyo;
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148; kilipatikana kiasi cha sh.48.977bilioni
b. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;kilipatikana kiasi shilingi 131.686 bilioni
c. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147; kilipatikana kiasi cha shilingi 510.017 bilioni
d. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220; kilipatikana kiasi cha shilingi 155.893bilioni
e. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82 ;kilipatikana kiasi cha shilingi 28.213 bilioni
f. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168; kilipatikana kiasi cha shilingi 19.710 bilioni
g. Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA, 392;kilipatikana kiasi cha shilingi 123.725 bilioni
Hali hiyo ilifanya marekebisho yote ya sheria za Kodi zilizofanywa katika mwaka huo wa fedha kuiwezesha serikali kukusanya jumla ya shilingi 1.018 Trilioni katika mwaka wa Fedha 2013/2014 na hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Hansard ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Hali hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Hapa tumezungumzia Wizara tatu tu za serikali kuu bado wizara 30 na idara mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Halmashauri na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ripoti hizi zimezidi kudhihirisha kwa mara nyingine kuwa matatizo yanayowakabili Watanzania ikiwa ni pamoja na umaskini, maradhi, ujinga yanaendelea kudumu kwa sababu watawala wa Serikali ya CCM wameamua yaendelee kuwepo kwa kukumbatia adui wa nne ambaye ni ufisadi.
Ripoti hizo za CAG ambazo zimeanika ufisadi katika maeneo yaliyokaguliwa ikiwemo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, kwa mara nyingine zimedhihirisha wazi kile ambacho CHADEMA kimekuwa kikisema kwa muda mrefu kwamba ufisadi huu unaoendelea kulitafuna taifa na kuwafanya Watanzania wazidi kuwa maskini ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mikakati na mipango ya CCM.
Wakati kasi ya ufisadi inaongezeka kutoka mwaka hadi mwaka kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete chini ya usimamizi wa CCM, ndivyo serikali hiyo hiyo inaongeza kasi ya kushindwa kusimamia UWAJIBIKAJI ambayo ndiyo moja ya nguzo muhimu katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaonekana katika kuboresha maisha ya wananchi hususan kuweka fursa za kujitafutia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hatimaye ustawi wa jamii nzima.
Ufisadi huu hauvumiliki tena. Watanzania wasikubali kuendelea kubeba mizigo ya watawala walioshindwa kutekeleza wajibu wao. Hali ya siasa inazingirwa na sintofahamu kubwa. Uchumi unazidi kuyumba. Kijamii, maisha yazidi kuwa magumu na walioko madarakani wamelewa madaraka. Msamiati wa UWAJIBIKAJI haumo vichwani mwao tena.
Ni mwaka wa Watanzania kuamua kuachana na ufisadi huu.
Imetolewa leo Jumatano, 20 Mei, 2015;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano- CHADEMAWEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment