Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, alipoulizwa na mwandishi wetu jana, alithibitisha kuwa jeshi hilo linazo taarifa za uwekezako wa kuwapo kwa ugaidi.
Alisema hata hivyo kuwa tayari wameshajizatiti na wameshatoa maelekezo kwa polisi waliopo mikoa yote nchini kuimarisha ulinzi.
Alisema kwa sasa wanaendelea kufuatilia kwa undani zaidi taarifa walizonazo kama ni za kweli au la.
“Baada ya kupokea taarifa hizi (bila kusema chanzo chake), tumejiimarisha na tumeshatoa maelekezo kwa polisi wetu waliopo mikoa yote wachukue tahadhari kwenye maeneo yao,” alisema na kuongeza:
“Kila taasisi ya usalama imepata ujumbe huu wa uwezekano wa Tanzania kushambuliwa na magaidi, kila mmoja anafuatilia kama ni kweli au uongo,” alisema.
Mangu amewaomba wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya usalama pale wanapohisi tofauti kwenye maeneo yao ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema kabla ya hatari.
Tishio hilo kupitia ujumbe uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, lilienea jana katika mitandao mbali mbali na Jeshi la Polisi limethibitisha kupata ujumbe huo.
Moja ya ujumbe uliozagaa kwenye mitandao ya kijamii ni ule unaosomeka:
"The Australian, UK and US governments have issued an enhanced terrorist alert for Uganda.
"Al Jazeera TV have intimated possible attacks in Mwanza and Dar es Salaam in Tanzania.
For information, James Ferdinand of UNAS Security and ATN Officer at the Philippines Embassy in Nairobi, Kenya, can be contacted. Friend please forward this sms to all your friends in Dar and Mwanza"
Ujumbe huo kwa tafsiri yake unanaanisha kuwa;
"Serikali za Australia, Uingereza na Marekani zimetoa tahadhari ya kufanyika kwa matukio ya ugaidi nchini Uganda.
"Televisheni ya Al Jazeera imetoa tahadhari ya uwezekano wa kuwapo kwa mashambulizi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Kwa taarifa James Ferdinand wa Shirika la Usalama la UNAS na Ofisa wa Ubalozi wa Filipini jijini Nairobi, Kenya, wanaweza kutafutwa kwa ufafanuzi.
"Rafiki tafadhali sambaza ujumbe huu kwa marafiki zako wote wa Dar es Salaam na Mwanza".
Wakati Mangu akitoa tahadhari hiyo, Msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba, juzi katika taarifa yake, alisema wameimarisha ulinzi kwenye maeneo yote yakiwemo yale ya kuabudia ambapo huwa na mkusanyiko ambao magaidi wamekuwa wakiitumia kufanya mashambulizi yao.
Maoni ya Wadau
Miongoni mwa wadau waliozungumzia tishio hilo ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wanachi (CUF) Julius Mtatiro, anayesema ana wasiwasi ndani ya nchi kuna kundi la watu linalojiandaa na matukio ya kigaidi, kutokana na mfululizo wa matukio ya kupora silaha kutoka kwa polisi.
Alisema jeshi la polisi pekee halitaweza kukabiliana na hatari hiyo kutokana na matukio ya hivi karibuni katika mikoa ya Tanga na Pwani, kuonyesha kuzidiwa kiasi ambacho ilibidi kuomba msaada kutoka Jeshi la Wananchi (JWTZ), kukabiliana na makundi ya watu wanaodaiwa kuwa zaidi ya majambazi.
“Uvamizi wanafanyiwa askari wetu, wanauawa na kuporwa SMG’s, napata shaka kuwa kuna kundi liko mahali linakusanya silaha taratibu na kujiandaa na uvamizi mahali,” alisema Mtatiro.
Alisema kutokana na magaidi kugeukia vyuo vikuu kama sehemu za mashambulizi, serikali inapaswa kuweka ulinzi mkali ili visishambuliwe.
Alisema kwa mtazamo wake anaona bado nchi inakabiliwa na ulinzi wa kuamini Mungu kutokana na maeneo ya vyuo kuwa rahisi kupitisha silaha hadi mabwenini.
“Utachoka pale ukiingia Mabibo Hostel na kitu chochote utapitisha tu. Hizi ni hostel na vyuo ambavyo vinalindwa na askari wa makampuni binafsi wasio na silaha au wakiwa na silaha duni," alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dare s Salaam, Dk. Benson Bana, alisema serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuacha tabia ya kupuuza kila jambo wanalosikia.
“Suala la ugaidi ni jambo zito ambalo huwezi kuliacha hivi hivi tu, tumeona wenzetu Uganda walivyochukua hatua na sisi tusizembee tuhakikishe ulinzi unawekwa kila mahali," alisema.
Alisema suala la ugaidi halitoki nje ya nchi pekee kwani hata ndani kuna uwezekano kuna watu wanaotumika na lazima tufikie mahali tuweze kutambuana ili iwe rahisi kuzuia jambo baya.
Leo wakristo Tanzania wanaungana na wenzao duniani kusherehekea sikukuu ya Pasaka.
Siku tatu zilizopita, wanamgambo wa Kisomali walifanya shambulizi Chuo Kikuu cha Garissa, kilichopo nchini Kenya na kuwaua watu 147.
Wanamgambo hao ambao wakati wakivamia kampasi ya chuo hicho, walikuwa wameficha nyuso na kujifunga milipuko kwenye miili yao na silaha, walirusha maguruneti na kumimina risasi dhidi ya wanafunzi.
Shambulizi hilo lililodumu takriban saa 15, awali lilifanyika bila kuchagua lakini baadaye baadhi ya Waislam waliachiwa na kuelekeza mashambulizi kwa Wakristo. WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment