CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewatoa hofu
wanachama wake mkoani Shinyanga kikidai propaganda zinazoenezwa na
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, anayedai
chama hicho kimepoteza mwelekeo si za kweli bali ni uongo.
Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu
ya CHADEMA Taifa, Bw. Godbless Lema, aliyasema hayo hivi karibuni mkoani
Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya
Mahakama ya Mwanzo.
Alisema chama chao bado kipo imara na hakitagawanyika kama
inavyodaiwa na Bw. Kabwe ambaye CHADEMA kilimfukuza katika chama baada
ya kukisaliti hivyo kukiuka Katiba ya chama hicho.
"Ndugu zangu wana Shinyanga, CHADEMA tupo imara na
tutaendelea kuwa imara hadi tukamate dola na kuwakomboa Watanzania ambao
wanateseka tangu tupate uhuru.
"Zitto hana ubavu wa kukigawa chama chetu kama
anavyofikiri na kuamini...anahangaika bure, alitaka kukiua tukamshtukia
na mimi ndiye mtu wa kwanza kubaini njama zake na wenzake akiwemo Samson
Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo; hivyo hawatubabaishi kwa lolote," alisema.
Bw. Lema aliongeza kuwa, Bw. Kabwe alikuwa chanzo cha
kufifisha ushindi wa CHADEMA katika baadhi ya majimbo katika Uchaguzi
Mkuu wa 2010 baada ya kutoa taarifa za uongo kwa wasimamizi wa uchaguzi
katika majimbo ya Katavi, Musoma Vijijini na Singida Mjini na
kusababisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama
hicho Taifa (BAVICHA), Patrobass Katambi, aliwataka wanachama wa CHADEMA
kusimama imara ili kukiimarisha chama chao na waachane na Bw. Kabwe
aliyeonesha dhahiri usaliti wake baada ya kujiunga na Chama cha
ACT-Wazalendo.
"Huyu Bw. Kabwe alikana katakata kujihusisha na Chama
cha ACT-Tanzania kama kilivyofahamika awali; lakini siku chache baada ya
kutimuliwa CHADEMA akajiunga nacho.
"Anawadanganya Watanzania kuwa yeye ni mjamaa na moja ya
sababu iliyomtoa CHADEMA ni kutokuwepo demokrasia ya kweli...kama kweli
anathamini demokrasia mbona baada ya kujiunga na ACT ghafla
amejitangazia madaraka ya Kiongozi Mkuu wa chama," alihoji Katambi.
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimetoa wito kwa wakazi wa
Mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu
la Wapigakura waweze kupata haki yao ya kuchagua viongozi waadilifu
katika Uchaguzi Mkuu.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment