MWANANCHI
Watu watano wamefariki dunia kutokana na
mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, watatu kati yao
wakiwamo wanafunzi wawili, wakipoteza maisha baada ya kibanda
walichojihifadhi kujikinga na mvua kuangukiwa na nguzo ya umeme na
kuwaunguza.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Temeke, Zakaria Sebastian alisema vifo vya watu hao watatu vilitokea katika eneo la Mchikichini Kimbangulile, Mbagala.
Sebastian aliwataja waliokufa kuwa ni Ramadhan Said (10), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Mchikichini, Alhaji Jumanne (15), mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Charambe na Monica Elistone (26).
Alisema wakati mvua ikiendelea kunyesha,
watu hao walijihifadhi kwenye kibanda kilichotengenezwa kwa mabati na
ghafla waya wa nguzo hiyo ulikatika na kuangukia kibanda hicho na
kushika moto.
“Wakiwa kwenye banda hilo, ghafla nguzo ilianguka na waya wake kuangukia kibanda kilichoshika moto na kuwateketeza watu hao,” Sebastian.
Mjumbe wa shina namba nne wa mtaa huo,
Kondo Namna alisema zaidi ya nguzo saba zimeinamia kwenye nyumba za
watu na wameshatoa taarifa Tanesco, lakini hadi jana, hakuna hatua
zozote zilizochukuliwa na shirika hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura
alisema wakati mvua zinaendelea kunyesha saa sita usiku wa kuamkia
jana, mkazi wa Mwananyamala Edward Warioba (22) alifariki dunia baada ya
kuangukiwa na ukuta akiwa amelala nyumbani kwake.
Katika tukio jingine, Kamanda Wambura
alisema maiti ya mwanamume mwenye umri wa kati ya miaka 45 na 50
iliokotwa ikielea kwenye makutano ya Mto Goba na Makongo.
Alisema huenda mtu huyo alisombwa na
maji ya mvua katika eneo ambalo bado halijajulikana. Wakati maafa hayo
yakitokea, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa katika maeneo ya ukanda wa Pwani na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuwa makini.
MWANANCHI
Marais wa nchi sita za Afrika kesho
watakuwa na mkutano mkubwa jijini hapa, juu ya uwekezaji na uboreshaji
katika ukanda wa kati huku wakitarajiwa kujadili changamoto za kadhaa za
kiuwekezaji.
Marais hao ni Joseph Kabila wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Pierre Nkurunziza wa Burundi, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenyeji wao wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo wa siku mbili utaambatana na mdahalo baina ya viongozi hao na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mjadala wa viongozi hao utajikita katika
umuhimu wa ukanda wa kati ambao ni kiungo muhimu katika ukuaji uchumi
wa nchi hizo kwa kuwa husaidia katika uingizaji na uuzaji wa bidhaa
mbalimbali kupitia Tanzania kwa njia za maji, reli na barabara.
Nchi hizo zimekuwa zikiathiriwa na
gharama kubwa za uendeshaji biashara ambazo zinahusiana na bei kubwa ya
usafirishaji, vikwazo vya kibiashara, ucheleweshaji na gharama lukuki za
kiutawala zinazobadilika mara kwa mara.
Wakati wa mkutano huo, viongozi hao watafanya uzinduzi wa treni ya mizigo kuelekea Uganda, Rwanda na DRC.
Mkutano huo utafanyika majuma kadhaa
baada ya ule wa Ukanda wa Kaskazini kufanyika jijini Kigali, Rwanda,
ambao Rais Kikwete alialikwa na kuweka hisia tofauti kuwa huenda kuna
mashindano baina ya kanda hizo mbili.
Nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, DRC pia ni wadau wa ukanda wa Kaskazini.
Ripoti ya ufuatiliaji maendeleo ya
ukanda huo kwa mwaka 2013 iliyotolewa na Wakala wa Kuwezesha Biashara na
Usafirishaji katika Ukanda wa Kati (CCTFA), ilibainisha kuwapo mizani saba na vituo tisa vya ukaguzi vinavyochelewesha biashara.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa uingizaji
wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam uliongezeka hadi tani bilioni
11.3 mwaka 2013 kutoka tani bilioni 4.95 mwaka 2013 huku DRC ikiongoza
kupitisha mizigo yake baada ya mwenyeji, Tanzania.
Kama zilivyo nchi wanachama wa ukanda
huo, Tanzania imejiwekea malengo lukuki ya kuboresha ukanda wa kati
hususan reli ya kati baada ya kuifanya kuwa moja ya vipaumbele sita vya
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Baadhi ya wadau walisema Tanzania
haitakiwi kukata tamaa kutokana na changamoto inazokabiliana nazo katika
kutekeleza miradi ya ukanda wakati kwa manufaa yake na nchi jirani.
MTANZANIA
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, wamemchagua Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mwidau (CUF) kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.
Katika uchaguzi uliofanyika jana mjini hapa, Mwidau alichaguliwa na wajumbe wa PAC kwa kupata kura 15 dhidi ya mpinzani wake, Lucy Owenya (Chadema) aliyeambulia kura mbili.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa
mshindi wa nafasi hiyo, Mwidau alisema atafanya kazi iliyoachwa na Zitto
Kabwe wakati akiiongoza kamati hiyo kwa kuzingatia masilahi ya nchi na
siyo watu binafsi.
“Moto
ni uleule ambao umeachwa na mwenyekiti mtangulizi wangu, Zitto Kabwe, na
tutafanya kazi pale alipoishia maana nikiwa mjumbe wa kamati hii
tulifanya kazi kama ndugu wa familia moja.
“Zitto
na Deo Filikunjombe waliweka misingi imara katika PAC na hilo
tutaendelea nalo na tutafanya kazi kama jicho la Bunge kwa Serikali hasa
katika kusimamia na kulinda rasilimali za Watanzania ila tunawaomba
waendelee kutuamini,” Mwidau.
Alisema ingawa imebaki takribani miezi minne Bunge kuvunjwa, kamati yake itaendelea na ratiba yake ya mwaka iliyokuwa imepangwa.
“Kama mwenyekiti kazi yangu kubwa ni
kuiongoza kamati kwa mujibu wa taratibu, sisi tunakagua hesabu za
serikali kuu na mashrika ya umma.
Tunaangalia namna serikali inavyofanya kazi yake, tuna mpango wa kazi, ratiba ya mwaka mzima tutaendelea nayo,” alisema.
Alisema pia kuwa kamati itaendelea na msimamo wa uwajibikaji na uwazi ambao ulikuwa ukisimamiwa na Zitto.
Akizungumzia kuchaguliwa kwa Mwidau
kuongoza Kamati hiyo, Mwenyekiti wa zamani wa PAC, Zitto Kabwe
alimpongeza kwa kushinda nafasi hiyo akisema ana imani ataendelea
kusimamia mifumo ya uwajibikaji.
MTANZANIA
Serikali imesema imepata hasara ya zaidi ya Sh bilioni nane kutokana na risiti za ununuzi bandia.
Kauli hiyo ilitolewa Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alipozungumza katika majumuisho ya semina kwa wabunge kuhusu Mfumo wa Malipo nchini.
Mkuya alisema kutokana na mfumo wa
kutumia malipo hayo mtu huwasilisha risiti za orodha ya malipo mengi
ambayo kwa uhalisia hayapo.
“Ukichukua
ile risiti ukienda dukani unakuta hakuna risiti kama hiyo ingawa
inakuwapo orodha ya vitu vingi vilivyoainishwa kwamba vitanunuliwa,” Mkuya.
Aliwataka wabunge kuunga mkono Muswada wa Sheria ya mpya ya Mifumo ya Malipo ya Taifa inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.
Wabunge wakichangia katika semina hiyo, walitaka sheria hiyo mpya kudhibiti wizi wa fedha kupitia mitandao ya simu.
Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM),
alisema mbali na sheria hiyo kutungwa sasa, lazima Serikali ibebe mzigo
wa wizi kupitia kampuni ya simu, ambao umekwisha kufanyika hadi sasa.
“Watanzania wamekwisha kuibiwa sana kutokana na kufanya miamala mbalimbali kwa kutumia mitandao ya simu.
“Kwa
nini jambo hili linalohusu fedha za watu lilianzishwa bila kuaepo sheria
na nani ataubeba mzigo wa fedha za watanzania zilizoibwa na makampuni
haya,” alisema.
Mbunge wa Chonga, Haroub Mohamed Shamis
(CUF) alisema Watanzania wanaibiwa matirioni ya fedha kupitia mitandao
ya simu lakini Mamlaka ya Mwasiliano Tanzania (TCRA) imekuwa ikiirushia
mpira Benki Kuuya Tanzania (BoT) kwamba ndiyo inatoa leseni za fedha.
“Tanzania kuna takriban kadi za simu
milioni 30, kila mtu akiibiwa Sh 100 kwa siku basi tunaibiwa Sh tririoni
moja kwa mwaka,” alisema.
Mbunge wa Viti wa Maalum, Diana Chilolo (CCM), alilalamikia huduma za ATM kwamba huduma za VISA na Master Card hazifanyi kazi nje ya nchi.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete na Uhuru Kenyatta wa Kenya wameingilia kati mgogoro uliopo baina ya mataifa hayo mawili kuhusu masuala ya usafirishaji na utalii.
Makubaliano yaliyofanywa na marais hao
ni pamoja na Kenya kuruhusu magari ya Tanzania, yanayofanya safari za
kupeleka wageni na watalii, maarufu kama ‘Shuttle’ kuingia kupeleka na
kuchukua watalii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKNIA).
Makubaliano mengine ni kwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), kurudisha safari za ndege ya Shirika la Kenya (KQ) kutoka siku 14 za sasa hadi 42 za awali.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akizungumza na
waandishi wa habari juu ya kikao kilichowakutanisha marais hao wawili
jijini Windhoek, Namibia.
“Kuanzia
saa 10:00 leo hii (jana) magari yote ya Tanzania yana ruksa ya kuingia
Kenya kuchukua na kupeleka watalii katika uwanja wa Jomo Kenyatta na
ndege za Kenya kuanzia leo zitaruhusiwa kurusha ndege zake kama kawaida
kwa siku 42 badala ya 14,” Membe.
Aidha, Membe alisema katika kikao hicho,
walizungumzia mambo mawili muhimu ambayo ni sekta ya usafirishaji na
utalii, ambapo pia walikubaliana ndani ya wiki nne, Mawaziri wa Mambo ya
Nje wa nchi hizo waitishe mkutano utakaowajumuisha Mawaziri wa
Usafirishaji, Utalii na Maofisa kutoka katika ofisi za Marais.
Alisema kabla ya kutoa taarifa hiyo,
waliwasiliana na Mawaziri wa Uchukuzi na Utalii ambapo pia taarifa hiyo
imetangazwa kwa wakati mmoja hapa nchini na Kenya. Waziri Membe alisema
mkutano wa kwanza utafanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam, ambapo
alisema katika mkutano huo ndipo kiini cha mgogoro huo kitabainika.
“Tanzania
na Kenya ni ndugu, ni majirani tusikubali kuchonganishwa wala kuonesha
tofauti zetu waziwazi, kama zipo ni vizuri tukaitana na kuzimaliza kimya
kimya,” alisema.
Rais Kikwete na Kenyatta wamekutana
jijini Windhoek ambako walikwenda kuhudhuria sherehe za miaka 25 ya
uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa rais wa tatu wa nchi hiyo, Dk Hage
Geingob.
MTANZANIA
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amesema atafanya kazi kukijenga Chama cha ACT kama alivyofanya kazi akiwa CHADEMA.
Zitto
ametaja sababu tano zilizofanya avutiwe na Chama hicho kuwa ni pamoja
na misingi ya Chama hicho kujali maslahi ya Taifa, itikadi za Chama
hicho kukubaliana na ujamaa, pia kukubaliana na imani ya ACT
inayosimamia umoja.
Kuhusiana na ishu ya usaliti wake kwa CHADEMA Zitto Kabwe amesema; “Naombeni
mjaribu kufumba macho yenu mjiulize ni Mbunge gani katika Bunge hili
ametoa hoja ambazo zilikitikisa CCM. Mara mbili nimetoa hoja ya kutokuwa
na imani na Waziri Mkuu.. Mara mbili nimeng’oa Mawaziri wa CCM, wanane
2011.. Suala la ESCROW nimeng’oa Mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali.. swali la usaliti walitakiwa kuulizwa hao ambao wako Bungeni
hawafanyi kazi kuiwajibisha Serikali”—Zitto Kabwe.
Wakati wa Mkutano huo wa Zitto chama cha ACT kilivuna wanachama wapya zaidi ya kumi wakiwamo waliokuwa viongozi wa TLP, CHADEMA na CCM.
DIRA
Utafiti uliofanywa na Shirika la
Utangazaji la BBC unaonesha kuwa kati ya wanawake watatu Afrika mmoja
kati yao anatumia mkorogo, wanawake hao wanatumia vipodozi vikali vyenye
Mercury mara 60 zaidi ya kiwango ambacho kimekatazwa.
Katika tafiti za Shirika la Afya WHO 77%
ya wanawake duniani wanatumia vipodozi hivyo vya kung’arisha ngozi,
huku ikielezwa kuwa katika kila wagonjwa 10 wa saratani ya ngozi, wanne
kati yao hupata tatizo hilo kutokana na matumizi ya mkorogo.
“Baadhi
ya wanawake wamekuwa wakipata madhara kutokana na kutumia vipodozi
vyenye sumu kwa muda mrefu hivyo sumu wanayoitengeza kwa muda mrefu
ndiyo huleta madhara makubwa kiafya..” aliongea Gaudensia Simwaza, Afisa Uhusiano wa TFDA.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment