Mambo magumu yameibuka katika suala la kujadili uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, baada ya kutokea malumbano makali na vurugu huku idadi kubwa ya wabunge wakiitaka serikali kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe bungeni.
Wabunge wengi walisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha mpasuko na kuvunjika kwa amani nchini.
Aidha, wamesema suala la Mahakama ya Kadhi linataka
kufanywa kama mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania
urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu ili kutafuta kura za Waislamu.
Mvutano huo uliibuka jana wakati wa semina ya wabunge
kujadili Muswada wa Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 ambao ndani yake
kuna Muswada wa Mahakama ya Kadhi ambao umepangwa kuwasilishwa Aprili
Mosi mwaka huu siku ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina,
alisema Kamati ya Katiba Sheria na Utawala ilipowaita viongozi
mbalimbali wa dini kuzungumzia suala hilo Waislamu walitofautiana katika
suala la uteuzi wa Kadhi kufanywa na Mufti Mkuu wa Tanzania na wakataka
waelewane kwanza kabla ya suala hilo kupelekwa bungeni.
Alisema katika mkutano huo makundi 11 ambayo hayakubaliana
na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), walisema Muswada wa
Mahakama ya Kadhi uletwe bungeni baada ya kuridhiana kwa sababu
hawakubaliani na Bakwata ambalo kiongozi wake ni Mufti Mkuu wa Tanzania.
Walisema maaskofu walisema hawana tatizo na suala la
Mahakama ya Kadhi, lakini isiwe na muundo kama wa mahakama nyingine na
kwamba mawazo ya waasisi wa Taifa, hawakutaka serikali iwe na dini na
ndiyo maana hawakuruhusu mahakama hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu, alihoji
ni kwanini Mahakama ya Kadhi inataka kuundwa na kupewa jukumu Mufti
ambaye anatoka Bakwata ambayo ni taasisi binafsi na imesajiliwa na
Mamlaka ya Rita.
“Bakwata ni taasisi kama zilivyo taasisi nyingine, haikubaliki, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi suala la Mahakama ya Kadhi ili Waislamu wampigie kura kwa sababu anataka kugombea urais mwaka huu,” alisema.
Rukia alisema ni marufuku serikali kuwalazimisha Waislamu
kuwa chini ya Bakwata na kwamba Waziri Mkuu, Pinda anafahamu kwa kina
suluhisho na mvutano huo wa Mahakama ya Kadhi.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR), Moses Machali,
alisema suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuingizwa katika
mfumo wa mahakama za kawaida inajichanganya na ibara ya 19 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua
msikiti wa Gadaf alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi
lisihusishwe na serikali kwa sababu wapo watu wengine ambao kila mmoja
ana imani yake.
Alisema hatua ya serikali kutaka kuuleta muswada huo wakati
bado Waislamu wenyewe hawaelewani ni kuwakosea Waislamu na kwamba
inawezekana Waziri alilizungumzia suala hili sababu ya malengo yake ya
urais.
Machali alisema kama muswada huu utapelekwa Bungeni itatoa
fursa kwa madhehebu mbalimbali kila moja kuanzisha mahakama yake hali
itakayoleta machafuko nchini kwa kuwa nchi itakuwa katika mfumo wa
mahakama za dini.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu,
alisema muswada unapendekeza kutambua kitu ambacho mfumo wa sheria za
nchi hauna na kwamba uongo unaotumiwa na serikali ndiyo unafanya watu
wawe na hofu.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Ally Kessy, alisema: “Katika
nguzo tano za Kiislamu Mahakama ya Kadhi haipo, nguzo sita za imani pia
haipo, sasa inakuwaje wanadai kitu ambacho hakitambuliki katika nguzo
za kiislamu.”
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema
muswada wa Mahakama ya Kadhi urudishwe ukaboreshwe badala ya kuharakisha
kuupeleka bungeni wakati bado una utata hata kwa waislamu wenyewe.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambali Nyangwine, alisema
Muswada wa Mahakama ya Kadhi usimamishwe ukafanyiwe utafiti kwanza
kwa sababu ndani ya Waislamu wenyewe hawaelewani.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Wabunge wasipokuwa makini na suala la Mahakama ya Kadhi, Bunge litaingia katika historia kuvunjika kwa amani.
Selasini alisema serikali iachane na kutoa ‘jini’
lililofungiwa na waasisi Mwalimu Nyerere na Karume na kwamba tukifanya
mchezo nchi itabaki katika vipande vipande.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alisema jambo hili litaligawa Taifa na kwamba waasisi hawakuwa wajinga walipokataa serikali isiwe na dini.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa,
alisema nchi inaelekea kubaya kwani msingi wa kuleta Mahakama ya Kadhi
ni kutaka kuwachota Waislamu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Serikali kama imedhamiria kuleta Mahakama ya Kadhi
ilete katika utaratibu mzuri, lakini kwa huu utaratibu ni unafiki na
mwenyezi Mungu hapendi unafiki, tusiwahadae Waislamu,” alisema.
Khalifa alisema kwa hali ilivyo muswada huo haujaiva na kwamba usiletwe bungeni hadi hapo serikali itakapojipanga vizuri.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema),David Silinde, alisema
suala la imani siyo la chama cha kisiasa kwani suala la Mahakama ya
Kadhi litaipeleka nchi kubaya na inawezekana ikawa ndio mwisho wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
“Mnataka kutuvurugia nchi sababu ya kutafuta kura za
Waislamu, kwa hili Waziri Mkuu umechemka sana, nalisema hili kwa sababu
wewe Waziri Mkuu ndiye uliyeahidi kuleta bungeni Muswada wa Mahakama ya
Kadhi,” alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema yasifanyike masikhala mswaada huyo uwasilishwe bungeni.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM),Mchungaji Lackison Mwanjale,
alisema serikali ikajipange upya katika suala la Mahakama ya Kadhi
kabla ya kuuleta bungeni muswada kwani bado suala hilo halieleweki kwa
jamii.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM),Martaza Mangungu, alisema
hakubaliani na suala la Mufti kupewa jukumu la kuchagua Kadhi Mkuu
wakati Waislamu wengi hawakubaliani na Bakwata ambayo inaongozwa na
Mufti.
Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema
muswada wa Mahakama ya Kadhi wapelekewe wahusika kabla ya kuletwa
bungeni ili wajadiliane na kukubaliana mambo ya msingi wanayoona
yatawafaa katika uanzishwaji wa mahakama hayo.
Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Peter Kafumu, alisema
serikali imeshindwa kusimamia vizuri suala la uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi kwa kushindwa kuwaelimisha wananchi jambo hilo.
Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahaya Kassim Issa, alisema Waislamu wanataka Mahakama hiyo kwa kuwa wanakosa haki hivyo serikali iruhusu kuanzishwa kwake.
Pinda: Tutatafakari Upya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akihitimisha mjadala huo
alisema kulingana na maoni yaliyotolewa na Wabunge ameelewa kwamba bado
hakuna maelewano miongoni mwa Waislamu wenyewe na pia hakuna uelewa wa
jamii kuhusu suala hilo.
Alisema mambo yaliyowasilishwa kuhusiana na muswada huo ni
maamuzi ya Bunge Maalum la Katiba na siyo yake, bali anabebeshwa msalaba
tu kwa sababu alikuwa anaiwakilisha serikali.
Pinda alisema kutokana na hali hiyo, serikali itakaa
kushauriana tena na Spika pamoja na Rais waone wafanye nini katika jambo
hilo.
Vijembe na Matusi
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage,
wakati akichangia hoja hiyo alishindwa kuvumulia baada ya baadhi ya
wabunge kuingilia mchango wake kwa kumzomea na kusema maneno
yaliyomuudhi na kuamua kuwatolewa maneno ya kuudhi (matusi).
Mbunge wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir, aliwaita baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea wakati akizungumza kuwa ni ‘wapumbavu’.
Wakati wa majadiliano hayo ilipofika saa 8:17 wakati Mbunge wa Kisarawe, Jafo akiendelea kuchangia kulitokea vurugu ambazo nusura wabunge wapigane huku baadhi yao wakiamua kutoka ukumbini.
Kutokana na kutokuwapo hali ya utulivu ukumbini, baadhi ya
askari pamoja na maofisa usalama waliokuwapo nje, walilazimika kuingia
ndani kuhakikisha amani haivunjiki.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alituliza vurugu ukumbini kwa kuwataka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wakichangia.
Katika majadiliano wabunge zaidi 30 walichangia na zaidi ya
20 walikataa muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe Bungeni siku
ya Jumatano wiki hii.
Kabla ya kuanza majadiliano, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia,
alitoa hoja kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na
Utawala, William Ngeleja, kwamba wakati wa majadiliano waandishi wa
habari wasiwepo ukumbini kwa kile alichoeleza ni unyeti wa jambo hilo.
Hata hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini,Kessy, alisema
kama waandishi wataondolewa ukumbini naye atalazimika kuondoka huku
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akisema hakuna sababu ya
kuwaondoa waandishi kwa sababu jambo linalojadiliwa wananchi wanataka
kulifahamu kupitia vyombo vya habari.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment