YANGA imetamka kuwa haina lengo la moja kwa moja 
kuachana na mshambuliaji wao Mrisho Ngassa na katika kuthibitisha hilo 
kwa vitendo, tayari uongozi wa klabu hiyo umeweka mezani Sh. 80 Milioni 
wakimtaka asaini dili jipya la kumbakisha timu hiyo.
Mmoja wa mabosi wa klabu hiyo aliyeko katika kamati ya 
usajili amesema kuwa uongozi wao chini ya mwenyekiti wa klabu hiyo, 
Yusuf Manji hauna nia ya kutaka kumtosa Ngassa ambapo tayari 
wameshampatia ofa hiyo kuhakikisha anasaini mkataba mpya.
Bosi huyo alisema katika ofa hiyo, Ngassa amepewa 
masharti mawili muhimu ambapo ametakiwa kutumia sehemu ya fedha hizo 
kumaliza deni lake la benki analodaiwa huku mshahara wake wa Sh. Mil. 4 
ukibaki kama ulivyo.
Hata hivyo sharti hilo la mshahara linaenda tofauti na 
ofa ambayo Ngassa alitaka kupatiwa na klabu hiyo akitakia alipwe dola 
3,500 (Sh. Mil 6.5) kwa mwezi ombi ambalo uongozi wa Yanga umeligomea.
“Hatuna nia ya kumuondoa Ngassa kuna vitu ambavyo 
anakosea, anaongea sana, haangalii kwamba juhudi zetu tunazozifanya 
tumeshampatia ofa hiyo afikirie sasa kama kweli anataka kubaki hapa,” 
alisema bosi huyo.
“Tumempa hiyo ofa lakini tatizo lake ni moja anataka 
mshahara mkubwa sana, kiasi ambacho ametaka tumpatie ni kikubwa sana 
kama atakuwa muelewa katika hili atakubali kusaini.”
Ngassa amekuwa akionekana kujuta kwa maamuzi yake ya 
kukataa ofa ye kwenda El Merreikh ya Sudan iliyomtaka wakati akiwa Simba
 kwa mkopo akitokea Azam ili tu akipige Yanga na kukumbana na adhabu ya 
kuwalipa Wekundu wa Msimbazi fedha alizosaini awali kabla ya kukimbilia 
Jangwani..
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:
Post a Comment