Wabunge wanawake wenye muda mrefu bungeni pamoja na mke wa waziri mkuu,
Mama Tunu Pinda juzi walimuandalia sherehe ya kumfariji mbunge wa viti
maalum (CCM), Vicky Kamata baada ya harusi aliyotarajia kufunga wiki
iliyopita, kukwama.
Sherehe hiyo ya faraja, ilifanyika Hoteli ya Dodoma kati ya saa 1.00 jioni na saa 6.45 usiku juzi mjini hapa.
“Unajua hata yeye mwenyewe tulim-surprise (tulimshtukiza). Alijua kuwa
ni chakula cha jioni, lakini alipofika alikutana na muziki, kwaya na
wabunge wengine waliompokea kwa vifijo na nderemo,” alisema mmoja wa
wabunge waliohudhuria hafla hiyo. Sherehe hizo zilitumbuizwa na kwaya ya
kikiristo ya Mvuke ya kanisa la Anglican mjini Dodoma.
Alisema Vicky alijua kuwa amealikwa na mbunge wa viti maalum (CCM),
Magreth Sitta kwa ajili ya chakula cha jioni lakini alipofika aka kutana
na sherehe.
“Tuliona ni vyema kumuandalia sherehe kidogo ili kumpa moyo kwamba hayo
yametokea kwa sababu Mungu alitaka kumuepushia na mambo makubwa siku za
usoni,” alidokeza mmoja wa waliohudhuria sherehe hiyo.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria ni wabunge wa viti maalum kutoka CCM
ambao ni Magreth Sitta, Anna Abdallah, Felister Bura, Hilda Ngoye,
Agness Hokororo na Anastazia Wambura.
Wengine waliohudhuria ni Asumpta Mshama (Nkenge-CCM), Anne Kilango (Same
Mashariki-CCM) na Waride Bakari Jadu (Kiembe Samaki-CCM). Chanzo hicho
kilisema wabunge Anne Kilango, Magreth Sitta na Anna abdallah,
walielezea jinsi baadhi ya wanawake viongozi walivyokumbwa na mikasa
kama ya Vicky na wengine hata kuacha wakiwa makanisani.
“Wengine walieleza jinsi walivyoteswa na wenza wao na kwamba amshukuru
Mungu pengine amemuepushia mambo makubwa ambayo yangeweza kutokea kama
ndoa ingefungwa,”alisema shuhuda huyo.
Alisema sherehe hiyo ilikuwa kama ibada maana muda mwingi ulitumika
katika kumuhubiria Vicky na kumsihi asikatishwe tamaa na badala yake
asonge mbele.
Alipoulizwa kuhusu sherehe hiyo, Vicky alikiri kufanyika lakini akakataa kuielezea kwa kina.
“Mimi niliitwa kwenye chakula cha jioni lakini nilipofika pale
nistaajabu kukutana na sherehe,”alisema Vicky ambaye alikataa kuelezea
kwa kina kuhusu sherehe hizo.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment