Stori: Deogratius Mongela na Chande Abdallah
SIRI nje!
Sakata la mmiliki wa Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan iliyopo Ilala
Bungoni, Dar, Dk. Juma Mwaka ‘JJ Mwaka’ kufanyiwa ziara ya kushtukiza na
baadaye kudaiwa kumkimbia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla limechukua sura mpya huku
mambo mengi yaliyomponza yakifichuka, Risasi Jumamosi limechimba.
SOO LILIVYOKUWA
Siku chache
baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya
kushtukiza katika kituo hicho kinachosifika kwa kutoa tiba ya asili
badala ya hospitali (tiba mbadala), hasa kwa wanawake wanaosumbuliwa na
matatizo ya uzazi.
Katika hali
ya kushangaza, matatibu na manesi waliokuwa kazini walitokomea
kusikojulikana na kuwatelekeza wagonjwa, wakikwepa kuonana na waziri
huyo ambaye akiwa na msafara wake, walifanya ukaguzi wa kina kwenye
kituo hicho.
Kufuatia
kitendo cha Dk. Mwaka na wenzake kuingia mitini, Waziri Kigwangalla
alitoa amri ya kufungwa kwa muda kwa kituo hicho mpaka uchunguzi wa kina
utakapokamilika ili kuona kama huduma zinazotolewa zinakidhi vigezo na
ni salama kwa wagonjwa.
MITANDAO YAMCHOMA
Simulizi ya
jinsi tabibu huyo alivyosimamishwa kutoa huduma ili kupisha uchunguzi na
ukaguzi wa kina, inaanzia mbali ambapo kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya
kuaminika, chokochoko kuhusu huduma zake zilianzia kwenye mitandao ya
kijamii.
“Kwa kipindi
kirefu kulikuwa na makundi mawili yanayoshindana kwenye mitandao ya
kijamii. Kundi la kwanza ni wale waliowahi kutibiwa katika kliniki hiyo
na kufanikiwa kupona matatizo yao.
“Hawa
walikuwa wakimtetea kwamba anatoa huduma sahihi lakini kundi jingine ni
wale waliotibiwa na kupoteza fedha nyingi bila kupona matatizo
yaliyokuwa yakiwasumbua.
“Hawa ndiyo
waliochangia kwa kiasi kikubwa kuifumbua macho Serikali ya Rais John
Pombe Magufuli kwani walitaka dawa na huduma za Dk. Mwaka zichunguzwe
kwa vile walishapoteza imani naye,” kilisema chanzo chetu makini kwa
sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Gari lake, ania ya Range Rover-Sport SE
KUANIKA MAISHA YAKE MTANDAONI
Kwa mujibu
wa chanzo kingine, tabia ya Dk. Mwaka kupenda kuanika maisha yake kwenye
mitandao ya kijamii ni suala jingine lililomponza na kufanya watu
waanze kutilia shaka utajiri wake.
“Unajua Dk.
Mwaka na mkewe wamekuwa wakiposti kwenye mitandao ya kijamii, hasa
Instagram picha za magari yao ya kifahari anayomiliki likiwemo Range
Rover-Sport SE na hekalu (jumba kubwa la ghorofa) analoishi, lipo Mbezi
(Dar).
“Pia
walikuwa na kawaida ya kujisifia wanaposafiri kwenda nje ya nchi kufanya
shopping, hasa Dubai. Hicho pia kimemponza sana maana watu walianza
kufuatilia utajiri wao na pengine ndiyo waliomchongea serikalini,”
kilisema chanzo hicho kilicho karibu na familia hiyo.
VIPINDI RUNINGANI
Sababu
nyingine inayotajwa na vyanzo vyetu kwamba imemponza tabibu huyo, ni ile
kawaida yake ya kuendesha vipindi kwenye runinga, akieleza huduma
anazozitoa kwa lengo la kupata wateja wengi.
“Unajua
Dokta Mwaka ndiye anayeongoza kwa kuwa na vipindi vingi vya runinga
kwenye televisheni mbalimbali nchini. Kama unavyojua kipindi kimoja cha
runinga kulipia kinagharimu fedha nyingi sana. Sasa watu wakawa
wanajiuliza anapata wapi fedha za kulipia gharama hizo? Ni kutoka kwa
wateja wake kweli?” kilisema chanzo chetu.
KUPUUZA AGIZO LA WIZARA
Pia, habari za ndani zinadai kuwa, mwaka jana wizara husika iliwaita wataalam wote wanaotoa tiba mbadala na kuwapa masharti.
Masharti
hayo ni kutovaa koti jeupe, kutoning’iniza shingoni chombo cha
kusikilizia mapafu/mapigo ya moyo (stethoscope) na kutojiita madaktari
wakitakiwa kutumia utambulisho wa tabibu masharti ambayo karibu wote
wameyapuuza.
KUNA KOSA KUJITANGAZA?
Katika
utafiti uliofanywa na gazeti hili na kutiliwa nguvu na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu imebainika
kwamba, kwa mujibu wa viapo wanavyokula madaktari na matabibu ni makosa
kujitangaza kwenye redio, runinga au mitandao kwa lengo la kuwavuta
wagonjwa.
“Changamoto
iliyopo kwetu ni kwamba matangazo wanayoyatoa ni kinyume na kanuni
lakini tumebaini kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo
inasimamia sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini ndiyo inayoruhusu.
Tumejipanga kukutana nao ili kujadili jambo hili,” alisema Mwalimu.
SIYO MARA YA KWANZA KUFUNGIWA
Tukio hili
la kusimamishwa kutoa huduma, si la kwanza kumtokea Dk. Mwaka ambapo
mwaka jana, maafisa kutoka wizara ya afya walifika kwenye kliniki hiyo
kwa kushtukiza, wakiwa wameongozana na waandishi wa habari na kufanya
ukaguzi ambapo kutokana na kutoridhishwa na mazingira waliyoyakuta,
walilazimika kuifunga kliniki hiyo kwa muda usiojulikana.
Hata hivyo, wiki kadhaa baadaye, Dk. Mwaka alifungua kesi mahakamani kupinga kufungiwa huko na kushinda kesi.
GPL
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment