HATIMAYE familia ya denti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, marehemu
Sekabenga Pius Mwakimenya (21) kilichotokea hivi karibuni na kugubikwa
na utata, imeanika ukweli kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na Uwazi, mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili, baba mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la
Joseph Mwigune alisema, taarifa waliyopewa na daktari aliyemfanyia
uchunguzi inamaliza utata na minong’ono yote inayoendelea chuoni.
Alisema, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kifo cha Sekabenga kimetokana na
mzunguko wa damu katika mishipa kutokuwa sawa, jambo lililosababisha
ajisikie vibaya na hatimaye kufariki dunia
“Daktari amesema kwamba mishipa ya damu haikuwa ikifanya kazi vizuri
hali iliyomsababishia ajisikie kuchoka kwa sababu damu haikuwa ikifika
sehemu zote za mwili wa marehemu,” alisema Mwigune.
Uwazi lilifunga safari hadi chuoni na kuzungumza na baadhi ya wanafunzi
ambao walionyesha wasiwasi kuwa huenda marehemu aliamua kujiua kwa sumu
kwa maelezo kuwa, siku chache kabla ya kifo chake alionekana mwenye
mawazo mengi.
“Hakuwa mwenye furaha, ni kama alikuwa na jambo zito linalomsumbua ndiyo
maana unasikia wanafunzi wengi hapa chuoni wanahusisha kifo chake na
sumu,” alisema denti mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa familia inayonukuu ripoti ya daktari
inaziba minong’ono yote kwa kuwa haionyeshi mahali popote kuwa marehemu
alijiua kwa sumu.
Marehemu Sekabenga alikuwa mwaka wa pili chuoni hapo akichukua Shahada
ya Kwanza ya Biashara na Uhasibu, mwili wake umesafirishwa Jumamosi Mei
31, mwaka huu kwenda mkoani Mbeya kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika
jana Jumatatu.
Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment