Mfanyabiashara huyo, Yusuph Barakati Saleh alikamatwa na TRA akidaiwa kumiliki mifuko 896 ya sukari iliyoingizwa nchini kupitia bandari bubu katika Kijiji cha Njianne, Kilwa mkoani Lindi.
Hatua hiyo imekuja takriban miezi miwili baada ya Rais Magufuli kutangaza kwamba hakuna vibali vitakavyotolewa kuruhusu uingizaji wa sukari, ili kuvilinda viwanda vya ndani.
Sukari hiyo iliyoingizwa nchini kutoka India na Brazil, ilikamatwa na timu ya doria ya TRA (Fast) usiku wa kuamkia Jumatano.
Timu ya Fast na Polisi ilibaini shehena hiyo ikiwa imehifadhiwa katika ghala, sehemu ikiwa imebadilishwa vifungashio na kutumia mifuko yenye nembo za viwanda vya Kilombero, TPC na Mtibwa ili ionekane imezalishwa nchini na kuingizwa sokoni.
Pia ilikuwapo sukari ambayo haikuwa imefungwa kwenye mifuko, bali ilikuwa imerundikwa kwenye turubai ikionekana kulowa maji.
Mwandishi alishuhudia sehemu ya sukari hiyo ikitiririka maji ya rangi ya kahawia, na ilidaiwa kuwa maji hayo yamekuwa yakikusanywa na kuingizwa sokoni kama asali.
Pia katika eneo hilo zilikamatwa bidhaa nyingine ambazo ni katoni 223 za betri za redio aina ya Tiger, katoni 135 za hamira na katoni 48 za sabuni.
Katika ghala jingine ambalo inasadikiwa ndimo shughuli ya kubadilisha vifungashio hufanyika, vilibainika vifaa mbalimbali kama mashine ya kusaga, jenereta, mzani, malighafi za kutengenezea mifuko na mashine za kushonea mifuko hiyo.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema bidhaa hizo zilikamatwa na kikosi hicho cha Fast, ambacho hufanya doria maeneo mbalimbali na kukamata bidhaa za magendo kwa kushirikiana na polisi.
“Kazi hii imetokana na juhudi za wananchi wema ambao wametupa taarifa na kikosi chetu cha Fast kwa kushirikiana na polisi wamebaini kwamba vitu hivi viko hapa,” alisema Kayombo. Alisema ghala hilo liko chini ya ulinzi na mzigo wote ambao umekamatwa utataifishwa na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.
Kayombo alisema pia ilikamatwa mifuko mitupu 2,000 yenye uwezo wa kujaza kilo 25 kila mmoja na mingine 36, 000 ya kilo 50 kila mmoja.
Alisema pia kuna mifuko 1,150 ya viwanda vya Tanzania iliyotumika ya kilo 25 kila mmoja, madumu matupu ya mafuta ya kula 609 ya lita 20 kila moja na mengine 310 ya ujazo wa lita 10 kila moja.
Akizungumzia athari za bidhaa hizo, Kayombo alisema kuwa ni pamoja na madhara ya kiafya kwa watumiajai na kwa uchumi kwa kuwa Serikali inapoteza mapato.
“Hatuwezi kuwa na uhakika wa ubora wa sukari hii maana itakuwa haijapita Shirika la Viwango (TBS), wala Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA),” alisema Kayombo.
Kayombo alisema TRA inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na bidhaa za magendo ambazo huingia kupitia bandari 11 bubu zilizomo wilayani humo.
Bandari hizo ni Kilutu, Kiheli, Sueli, Shuka, Mayungiyungi, Milamba, Mapimbi, Limayao, Kisongo, Kimwera na Nchinga.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho alisema kuwa amemfahamu mfanyabiashara huyo na shughuli hizo tangu mwaka 2008 na amekuwa akishusha mizigo hiyo wakati wowote, huku vijana wakijipatia ajira za muda.
“Huyu jamaa alikuwa hachagui muda wa kuleta mizigo, alikuwa akileta muda wowote, usiku na mchana kwa sababu hapakuwa na mtu wa kumghasi,” alisema mkazi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Alisema mfanyabiashara hiyo amekuwa anawauzia bidhaa hizo wenye maduka na hata wanakijiji wamekuwa wakinunua sukari hiyo.
Mkazi mwingine alisema licha ya kumuona mfanyabaishara huyo akishusha mizigo yake mara kwa mara, alikuwa hajui kama bidhaa hizo ni za magendo.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment