Kingunge Ngombare Mwiru, ambaye ni kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametabiri anguko na mpasuko mkubwa ndani chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, endapo chama hicho kitaacha kumpitisha mgombea urais anayekubalika kwa wananchi wengi.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya jina la Edward Lowasa kuenguliwa kutoka majina matano yaliyopendekezwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC- NEC).
Kutajwa kwa majina ya Bernard Membe, Dk. John Magufuli, Amina Salum Ali, January Makamba na Dk. Asha-Rose Migiro na Kamati kuu kwamba ndio watajadiliwa na Halmashauri Kuu (NEC), kumemfedhehesha Kingunge hata kusema, “…hatua ya kwanza itakuwa kumweka mgombea ambaye hakubaliki ndani ya chama na hakubaliki nje ya chama. Itakuwa ni kura ya hasira.”
Kingunge ametoa kauli hiyo kwa kusitasita huku akionekana kuwa na huzuni wakati akifanya mahojiano na kituo cha Azam Tv leo mchana.
Japo Kingunge hakutaja jina la Lowassa lakini ni muungwa mkono katika mbio zake za kuusaka urais hata wakati wa mkutano wa kutangaza nia mjini Arusha Kingunge alisema, “…Lowassa ndiye pekee anasifa za kuwa rais wa Tanzania.”
“Utaratibu wa mwaka huu una matatizo. Kilichotokea ni mazingira yanayotia shaka. Kwa sababu ya muda hakuna atakae kata rufaa. Inaonesha kwamba uongozi umeshakuwa na msimamo juu ya mgombea wanaemtaka,” amesema Kingunge.
Amesema kazi ya CC-NEC ni kuyapitia, kuangalia sifa, kuwapima, kuyalinganisha na kisha kutoa mapendekezo. "Hawana madaraka ya kuamua."
Kuhusu kukubalika kwa majina hayo na NEC, Kingunge amesema, “…wajumbe wa NEC wanaweza kukubaliana nayo, wanaweza kusema hapana, wanaweza kusema wote waliopendekezwa hawafai na wanaweza kutoa mapendekezo waletewe majina mengine.”
Amesema kuwa yanayotokea sasa na yatakayotokea baadae ni mazingira ambayo yamekuwa yakijengwa kwa muda mrefu na viongozi wakuu wa chama.
Kuhusu sifa za mgombea anayemtaka, Kingunge amesema ni lazima: Aweze kupambana na nguvu ya upinzani; anayekijua chama; awe na uzoefu wa masuala ya ulinzi na usalama na mtu atakae watoa watanzani kwenye umasikini.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment