Kama waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa asingehusishwa na sakata la Richmond kwa namna washindani wake kisiasa wanavyolazimisha, sakata lingeendelea kuzungumzwa?
Maswali haya mawili yana majibu yake sahihi kwa wanaojua undani wake, akiwemo Lowassa aliyejiuzulu ili kulinda heshima na mustabali wa nchi, serikali na chama cha mapinduzi-CCM, kama anavyonukuliwa akisema. Yawezekana amelinda maslahi ya nchi kwa vile wahisani hawakusitisha misaada yao muhimu kwa bajeti ya nchi.
Kwa muktadha wa makala na ulinganifu wenye mantiki, hakuna manufaa makubwa kwa umma kupigia kelele Richmond iliyopitia Dowans na kubaki Symbion Power na kujisahalisha huu ubadhirifu na upotevu mkubwa wa fedha za umma unaobainishwa kila mwaka na CAG bila kufanyiwa kazi ipasavyo kwa hatua stahiki dhidi ya wahusika.
Hizi mbinu za kisiasa za kukumbuka Richmond ili kutimiza malengo ya baadhi ya wanasiasa ya kulazimisha na kuwaaminisha watu mambo yawe watakavyo yanazidi kufifia na kushindwa kadri siku zinavyozidi kubadilika.
Eti wanakumbuka sana Richmond kwa vile imehusishwa na Lowassa!!!
Sina nia ya kumsafisha mchafu yeyote wala kumchafua msafi bali nauzungumzia uhalisia tu.Unawezaje kukumbuka Richmond na kukataa kuona ubadhirifu unaoibuliwa na CAG anapoonyesha zaidi ya sh. trion moja zimeyeyuka serikalini?!
Kama ilivyokuwa Richmond na waliouaminisha umma iwe watakavyo katika bunge la kasi na viwango la Spika Smweli Sitta ndivyo ilivyotokea kwa sakata la Tegeta Escrow ambapo wanasiasa wamethubutu kutoa hukumu wanayolazimisha iwe dhidi ya wale walioitwa mafisadi, na kuimiminisha dhana husika kwa wananchi.
Baadhi ya wahusika waliojiuzulu kutokana na sakata la Esrow kama njia ya kuonyesha uwajibikaji kisiasa wamethibitika kutohusika. Kati yao ni aliyekuwa waziri wa nishati na madini Profesa Sospeter Muhongo na katibu mkuu wake Eliakim Maswi, ambao kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza uhusika wao haikuona hatia yoyote dhidi yao.
Bahati mbaya, enzi za Richmond hakukuwa na kamati maalumu ambayo ingethibitisha, kwa mfano, usafi wa wanasiasa waliohusishwa na Richmond baada ya kujiuzulu kwao.
Sijui wanasiasa wanaoshupalia Richmond wakidhani kuikumbuka kwa kutaathiri safari ya kisiasa ya Lowassa wakiambiwa ukweli tofauti watatumia kete gani mpya kujipandisha kisiasa.
Wanasiasa wenye "homa ya Lowassa" wanaamini kete pekee ya kufifisha umaarufu, kukubalika na safari ya matumaini ya Lowassa ni kutumia sakata la Richmond.
Bahati mbaya ya makusudi kwao ni kutowaambia wananchi ile Richmond wanayojikumbusha hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu octoba mwaka huu, ndiyo hii Symbion ambayo Rais wa Marekani Barack Obama anaijua na anaamini kazi inayofanywa nayo ndani ya Tanzania katika sekta ya Nishati.
Sasa wewe mwanasiasa ukiikumbuka Richmond, unganisha Dowans ili uiseme Symbion kwa sauti ya juu itakayowafikia wananchi ili waweze kukuuliza umefanya nini au unakumbuka yapi angalau kimya kimya kuhusu EPA,Kagoda,Meremeta,Deep Green Finance,Tegeta Escrow; unachukuliaje ripoti mpya ya CAG na uamuzi wa wahisani kusitisha misaada muhimu ya kibajeti kwa nchi.
Hadi sasa kunawatu hawako tayari kusikia tofauti na walivyoaminisha au kuaminishwa juu ya Richmond.
Pengine ule msemo apendao kuutumia Rais Kikwete kwamba "Akili za kuambiwa changanya na za kwako" ni muafaka kuwagutusha watu ili wapambanue dhamira za wanasiasa kabla, wakati na baada ya kusikia wanenacho na watendacho.
Endapo wanasiasa watadhani siasa za kuchafua wagombea wanaotakiwa na wananchi walio wengi ili wao wasiotakiwa wabahatike kuteuliwa na vyama, yaliyomtokea Goodluck Jonathan na kilichokuwa chama tawala Nigeria si ajabu kujirudia kwa CCM. WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment