Lowassa ambaye alikuwa msaidizi wa Rais Kikwete kwa miaka miwili kama msimamizi wa shughuli za Serikali, amepingana na bosi wake akisema alikosea kuanza na kilimo kwanza na kuweka elimu kando.
Kauli ya Lowassa inakinzana na utaratibu wa CCM unaowataka viongozi kupingana au kukosoana kupitia vikao badala ya kufanya hivyo hadharani, hatua inayotafsiriwa kama kudhoofisha chama.
Badala yake, Lowassa ametamba kuwa, akiwa rais ataanza kushughulika na elimu kama lengo kubwa na sio kilimo kwanza cha serikali ya Kikwete.
Vigogo wengine wa CCM aliowashambulia ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeongoza Kamati teule, akisema wawili hao walipika ripoti ya kashfa hiyo ili kumdhalilisha.
Lowassa na makada wenzake watano, Fredrick Sumaye, Steven Wassira, Bernard Membe, January Makamba na William Ngeleja, waliondolewa kifungoni Mei 23 mwaka huu, baada ya kufungiwa kwa mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza mchakato mapema ndani ya chama.
Katika kile kilichoonekana kama kujibu mapigo ya tuhuma za ufisadi dhidi yake, Lowassa aliwaalika baadhi ya wahariri wachache kutoka Jukwaa la Wahariri nyumbani kwake mjini Dodoma leo, na kufafanua baadhi ya mambo kadhaa kupitia “wateule wake” hao.
Akizungumzia tuhuma za zabuni tata ya Richmond Development LLC, Lowassa amesema “sihusiki na lolote kuhusu sakata hilo na ndio sababu hata Kamati ya Mwakyembe haikunihoji.”
Amesisitiza kuwa, cheo cha uwaziri mkuu ndicho kilikuwa lengo la kamati ya Dk. Mwakyembe na Spika Sitta kumshughulikia.
“Hicho sio kikwazo kwangu katika kuingia Ikulu, kwani sakata la Richmond lilipikwa kunichafua. Nimechukua muda mrefu kuzungumzia hili la Richmond na nitalisema zaidi Arusha wikendi hii,” amesema Lowassa ambaye atatangaza nia ya kuwania urais siku hiyo.
Kuhusu kutumia makundi ya kumshawishi kutangaza nia, Lowassa amesema “naamini kila mtangaza nia ana makundi ya kumuunga mkono.”
Mkutano wake huo, mbali na wahariri pia ulihudhuriwa na Nazir Karamagi-mmoja wa mawaziri waliojiuzulu pamoja na Lowassa mwaka 2008 kwa kashfa hiyo, wabunge Peter Serukamba, Diana Chilolo.
Walikuwepo pia wafuasi wake wengine, Hussein Bashe, baadhi ya waliokuwa wakuu wa wilaya walioenguliwa kama Elibariki Kingu (Igunga) na aliyekuwa Mkurugenzi wa HakiElimu, Elizabeti Misoki.
Misoki ametangazwa rasmi kuwa mkurugenzi wa mahusiano na mawasiliano katika timu ya kampeni ya Lowassa. Amehoji kwani akina Karamagi wana tatizo gani na kwani wao sio binadamu?
Kuhusu mabilioni ya fedha anazogawa kwa baadhi ya makundi, Lowassa anasema anapata michango ya rafiki zake na kwamba ataendelea kupokea michango hiyo wakati wote wa harakati zake na haina madhara yotote.
“Sitahama CCM. Asiyenitaka ndiye aondoke kwenye chama kwani mimi nina uhakika wa kupata nafasi ya kuwania urais,” amesema.
Lowassa amefafanua kuwa, hatalipa kisasi kwa lolote lililomtokea katika siasa kwani, amemwachia Mungu kwa vile yeye ni mcha Mungu.
Ametamba kuwa Arusha itawaka moto tarehe 30 mwezi huu, na kuwataka Watanzania kutega sikio kwani ataanika kila jambo kuhusu mustakabali wa nchi hii na mipango yake ya kuiinua nchi kiuchumi katika miaka kumi ijayo. WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment