Sakata la nani mmiliki halali wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda),
limeendelea kuchukua sura mpya. Wakati Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas
Mtemvu akitoa tuhuma kwamba limeuzwa kinyemela, Mwenyekiti na Mkurugenzi
wa Simon Group, Robert Kisena ameibuka na kudai kuwa halikuwahi kuuzwa.
Juzi, akichangia mjadala wa Bajeti wa Wizara ya Fedha, Mtemvu alisema
kulifanyika ujanjaujanja kati ya Simon Group na Meya wa Jiji, Didas
Masaburi kukopa benki na taasisi nyingine kwa ajili ya kununua kampuni
hiyo.
Mtemvu alisema baada ya Simon Group kuuziwa Uda kwa bei poa, wahusika
walishindwa kulipa fedha hizo ndipo (wadai) walipokwenda mahakamani na
kutaka walipwe chao.
Alisema baada ya kampuni na benki walizokopa kushinda kesi mahakamani,
kampuni moja ya udalali ilipewa kazi ya kuipiga mnada depo ya Uda na
Februari 23, ilinunuliwa na Jazeera kwa Sh12bilioni.
Jana, Mtemvu alisema: “Tunaambiwa kulikuwa na zuio, hapa tunataka kujua,
kwanza huyu aliyeweka hati za Uda kwa zuio isipigwe mnada... utaratibu
uliotumika kuiuza Uda, hapa kuna mchezo mchafu umefanyika, iweje mambo
yafanyike bila wadau, wahusika wa mkoa kushirikishwa?”
Alisema Uda haiwezi kuuzwa kwa bei chee ya Sh280 milioni... “Ina viwanja
Stesheni, ina nyumba Msasani, Chang’ombe, Ilala Sharif Shamba,
Kijitonyama, Upanga hivi vyote ni zaidi ya Sh280 milioni.”
Katika maelezo yake bungeni juzi, Mtemvu alisema wabunge wa Dar es
Salaam hawakatai kubinafsishwa kwa Uda ila wanataka uhalali na haki
katika ubinafsishaji huo.
Kisena
Akizungumza jana, Kisena alisema Uda haijauzwa na hawana mpango wa
kuiuza na akahusisha tuhuma hizo na mkakati mbaya unaofanywa na baadhi
ya watu wasiopenda maendeleo ya shirika hilo.
“Mimi ndiyo kwanza nasikia habari hizo eti Uda imeuzwa kwa Kampuni ya Jazeera… sijui kwa nani… huo ni uzushi.
Nenda kwa Mtemvu akupe document (nyaraka) za uuzwaji wa Uda… akwambie
iliuzwa lini na kwa sababu zipi na kama iliuzwa kwa madeni ni benki gani
inadai ili uweze kufuatilia na kuuambia umma ukweli.”
“Watu wote watambue kuwa Uda inamilikiwa na watu wawili: Simon Group na
Serikali kupitia Msajili wa Hazina na hakuna mmiliki mwingine na
halijauzwa. Hii kampuni ni kubwa sana hivi iuzwe bila waandishi wa
habari na umma kujua na mnada hutangazwa siku 14 kabla… yaani siku zote
zipite watu wasijue?” alihoji Kisena.
Brela
wakati mvutano huo ukiendelea, Wakala wa Usajili na Utoaji wa Leseni za
Biashara (Brela), umesema hauna taarifa zozote za kampuni hiyo kuuzwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyus alisema jana kuwa ofisi yake
haina nyaraka zozote zilikuwa zikionyesha Uda kuwa iliuzwa kwa Kampuni
ya Jazeera.
“Tulisikia taarifa hizo lakini hatukupata document (nyaraka) zozote
zinazothibitisha jambo hilo. Nimewaomba maofisa wangu waendelee
kufutilia suala hilo na kama kuna chochote tutawajulisha,” alisema
Kanyus.
Sakata la Uda liliibuka tena juzi kwa Mtemvu na Mbunge wa Urambo
Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya kuchafua hali ya hewa bungeni kila
mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa anahongwa kutetea ufisadi katika shirika
hilo.
Mvutano huo umeibuka wakati Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge
ikiwa tayari imemhoji, Kisena baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika kusema aliingilia uhuru wa Bunge kuhusu mgogoro wa uwekezaji
katika shirika hilo.
Juzi bungeni
Juzi bungeni, Mtemvu alisema: “Kwanza niseme kitu kimoja kibaya sana,
humu ndani kuna mjumbe wa Bodi ya Uda (Profesa Kapuya), alikuwa
akizunguka sana humu ndani (ndani ya Bunge) huku akiwaona wa wabunge
kitendo hicho si kizuri.”
Alisema kuwa mwekezaji huyo wa Uda ameliuza shirika hilo kwa Sh280
milioni na kuhoji kama kiasi hicho cha fedha ni hadhi ya Uda na kuwa
mwekezaji huyo hakukabidhiwa shirika hilo na vikao halali vya jiji la
Dar es Salaam, bali na Meya wa Jiji.
“Tunapoongea tusiangalie sambusa za Dodoma Hotel, tuangalie uasilia wa
jambo, hivi tunauza mali ya Serikali bila Baraza la Mawaziri kujua?”
alihoji.
Mtemvu alikatishwa na taarifa kutoka kwa Profesa Kapuya ambaye alisema si haramu kwa mbunge kuwa mwekezaji.
“Sera inaruhusu kwa mbunge kuwa mfanyabiashara. Afadhali mimi
nimezunguka kuona watu kuliko anayezunguka kwa madhumuni ya kurudisha
imprest (masurufu),” alisema Profesa Kapuya.
“Na aliyezungumza ni mmojawapo (Mtemvu)… hakuna mali ya Serikali
iliyouzwa bila idhini ya Baraza la Mawaziri, zilizouzwa ni hisa za jiji
ambazo yeye alikuwemo katika kikao (Mtemvu)”alisema.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Sharon Sauwa, Habel Chidawali (Dodoma) na Nuzulack
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment