Najuta kumpa uhuru wa kidemokrasia tangu akiwa Shule ya Msingi. Kila akiniona ananitambia kuhusu UKAWA na kukwama kwetu kama CCM.
Nimejaribu kumwambia kuwa mimi sipo tena kwenye kampeni za CCM. Bado ananing'ang'ania. Ananibakisha CCM na kunihusisha moja kwa moja na kampeni za wagombea wetu kuanzia Dr.Magufuli, Mama Samia, wale wa Ubunge na Udiwani.
Nyumba yangu mwenyewe imegeuka uwanja wa tambo na vikumbo vya kikampeni. Yeye amejipambanua kuwa ni mfuasi wa UKAWA kupitia CHADEMA.
Leo, ameshanipigia simu kujiproud kuwa Lowassa anaibomoa ngome ya CCM pale Millenium Towers. Anadai kuwa Lowassa atawateka wanawake wa Tanzania na kuifanya CCM ibaki na wazee tu kama wapigakura wake.
Akajinasibu kuwa wanawake wa Tanzania wanaiacha mkono CCM na inaelekea kuyumba pamoja ya karata yake ya kumsimamisha Mama Samia kama mgombea mwenza.
Leo pia, amenidokeza kuwa watanzania hawa si wale. Amesema kuwa ana tafiti zilizo fiti zikionesha kuwa UKAWA ndiyo dawa. Ananisubiri anioneshe nikifika nyumbani jioni.
Lengo lake nalijua. Ni kuninyanyasa kisiasa lakini kisasa. Kwa hoja za haja bila kubadili lahaja. Najiandaa,kwa kujisomea nyaraka za haraka na baraka,kwenda kupindua tafiti zake. Nikifika nyumbani, kampeni za chumba kwa chumba zitaanza.
UKAWA mmeniharibia mwanangu. Kwasasa hadi ana kibwagizo chake: MAGUFULI APIGE KAMPENI, LOWASSA ATAPIGIWA KURA! Kazi kwelikweli.
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dar es Salaam WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment