Zitto Jana katika maziko ya Shida, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wa kuteuliwa na Rais, Zitto aliwataka wajumbe wenzake
kumuenzi mama yake kupitia viongozi wao, Mwenyekiti wa Kamati namba
nane, Job Ndugai na Mwakilishi wa Ukawa, Profesa Ibrahimu Lipumba.
Alitoa ujumbe huo nyumbani kwa marehemu mama yake, mtaa wa Kisangani
Mwanga, muda mfupi kabla ya kwenda makaburi ya Rubengela mjini Kigoma
ambako mwili wa Shida Salum ulizikwa. Zitto alisema kama kweli viongozi
hao wanataka kumuenzi mama yake, wamalize tofauti zao na kulifanya Bunge
Maalumu la Katiba, kuendelea na shughuli yake ya kuwaletea Watanzania
Katiba itakayowafaa kwa muda mrefu.
Alisema kuwa mama yake alikuwa mjumbe wa Bunge hilo baada ya kuteuliwa
na Rais Jakaya Kikwete, nafasi ambayo ingempa fursa ya kuandika historia
ya kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, katika kuandika Katiba mpya ya
Tanzania.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa mama yake aliugua na Mwenyezi Mungu kwa
kudra zake akamuondoa katika nafasi ya kuandika historia hiyo,
kilichobaki ni viongozi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kufikia
maridhiano na kuandika Katiba hiyo.
Zitto alisema amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kumsaidia mama yake
kupata matibabu ambayo yangerudisha afya yake, na kumpa fursa ya
kushiriki katika shughuli zake za kawaida, lakini Mungu alipitisha
uamuzi wake ambao hakuna wa kumpinga.
Naye Ndugai, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, aliyeongoza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwenye maziko hayo, alisema Shida alikuwa mtetezi wa Watanzania
wa hali ya chini.
Alisema yaliyotokea ni mapenzi ya Mungu na kuitaka familia wasihuzunike
kiasi cha kupitiliza, badala yake wakae pamoja na kuweka familia pamoja
na kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao ya Taifa.
Naye Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, alisema
kuwa Shida alisimama kuwapigania watu wenye ulemavu mchango ambao
alikusudia kuutoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo Lipumba alionya kuwa kama kweli watu wana nia ya kumuenzi
Shida, hawana budi kusikiliza maoni ya wananchi walio wengi katika
kuipata Katiba mpya, badala ya watu wachache kutaka kuichakachua.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment