WAHALIFU wa
mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za utupu na ngono, wasambazaji
wa taarifa za uwongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine ambao
wanafanya udanganyifu unaohusiana na kompyuta wametungiwa sheria kali
ambayo itawafanya kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini isiyopungua
Sh milioni 50.
Miongoni
mwa miswada ya sheria utakaowasilishwa bungeni na Serikali wiki hii
mjini hapa, ni Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo
imeainisha makosa mbalimbali yanayofanywa na wananchi katika kipindi
hiki ambacho matumizi ya mtandao wa kompyuta yameongezeka.
Baadhi ya
makosa yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo ni kughushi kunakohusiana na
masuala ya kompyuta, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, ponografia za
watoto, picha za utupu, matusi na ngono, makosa yanayohusiana na
utambuzi, uwongo, ubaguzi, matumizi ya kibaguzi, mauaji ya kimbari na
unyanyasaji kupitia mtandao wa kompyuta.
Katika
sheria hiyo, mtu atakayesambaza ponografia ya watoto kupitia mtandao wa
kompyuta atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50 au mara tatu
ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au kifungo kisichopungua
miaka saba jela au vyote kwa pamoja.
Mkosaji pia
ataamriwa kumlipa mwathirika fidia. Kwa upande wa kusambaza picha za
ngono, matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Sh milioni 30 au
kwenda jela miaka 10 au vyote.
Lakini mtu
atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh milioni 20 au
kwenda jela miaka saba au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Pia kweye
muswada huo mtu ambaye atatoa taarifa, data au maelezo kwa njia ya
picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo
akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh milioni 3 au kutumikia
kifungo jela kisichopungua miezi sita au vyote.
Kwa upande
wa ubaguzi, sheria hiyo inakataza mtu kutumia mtandao wa kompyuta
kutozalisha vitu vya kibaguzi kwa madhumuni ya kuvisambaza na iwapo
atatiwa hatiani atalazimika kulipa faini ya Sh milioni tatu au kifungo
cha mwaka mmoja jela.
Pia mtu
akimdhihaki mtu mwingine kwa kupitia mfumo wa kompyuta kwa mwelekeo wa
ubaguzi wa rangi, kabila, asili, utaifa au dini fulani akitiwa hatiani
atatozwa na Mahakama faini ya Sh milioni tatu au kifungo cha mwaka mmoja
jela au vyote kwa pamoja.
Pia sheria
hiyo inakataza mtu kuchapisha au kusababisha kuchapishwa vitu
vinavyochochea au kuhalalisha matendo yanayopelekea mauaji ya kimbari na
makosa dhidi ya binadamu kwa kupitia mtandao wa kompyuta.
Mtu
atakayefanya hivyo atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika
kulipa faini isiyopungua Sh milioni 10 au kutumikia kifungo
kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Pia muswada
huo wa sheria unakataza mtu kutoanzisha usambazaji wa taarifa
zinazotumwa bila ridhaa na ukitiwa hatiani utatozwa faini ya Sh milioni 3
au mara tatu ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au kutumikia
kifungo kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment