Wingu jeusi limeanza kutanda kuhusu hatima ya mzozo wa Ziwa Nyasa
kutokana na msimamo wa hivi karibuni wa kiongozi wa Democratic
Progressive Party (DPP), Peter Mutharika ambaye sasa ni Rais mpya wa
Malawi.
Hiyo inatokana na msimamo wa Mutharika ambaye ni Profesa wa Sheria wa
kupinga kuendelea kujadiliana na Tanzania kuhusu nani mwenye haki ya
kumiliki ziwa hilo alioutoa wakati alipowatembelea wananchi wa Chipoko,
kando ya ziwa hilo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu ambao
ulimwigiza madarakani.
Pamoja na kwamba mazingira ya msimamo huo yanaweza kutofautiana na hali
halisi ya sasa, tofauti za kisiasa baina yake na mtangulizi wake, Joyce
Banda zinaweza kuongeza msukumo mpya wa kutaka kutoendelea na mazungumzo
ya mpaka wa ziwa hilo.
Akizungumza na wananchi hao, Profesa Mutharika aliwatoa wasiwasi na
kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa maelezo kuwa ziwa
hilo lipo kwenye himaya ya Malawi na kwamba kuendelea kujadiliana na
Tanzania ni kupoteza muda.
“Hakuna haja ya kuendelea kujadiliana, Ziwa Malawi ni mali ya Malawi na
litaendelea kuwa la Malawi daima,” alisema Mutharika ambaye pia amewahi
kufundisha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alimshutumu Banda na kudai alikuwa dhaifu kiasi cha kutoa fursa kwa Tanzania kutumia udhaifu huo kutaka kupora ziwa hilo.
“Ziwa hili letu ila Tanzania inatumia tu udhaifu wa Serikali iliyopo
kwani wenyewe wanajua ndani ya mioyo yao kuwa hawana chochote katika
ziwa hilo. Tutakaporejea serikalini mwakani haya mambo yote yasiyo na
kichwa tutayamaliza. Nataka niwahakikishie kwamba tutapeleka meli zaidi
kwenye ziwa hili ili kuinua shughuli zetu za kiuchumi na kutengeneza
ajira kwa vijana wetu.”
Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali ya Tanzania ilitoa msimamo wake
kuhusu mzozo huo wa mpaka na kudaia kuwa itaendelea kujadiliana na
Malawi.
Akizungumza bungeni wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara yake, Waziri wa
Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema
Tanzania ilikuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi wa Malawi na kwamba
iko tayari kufanya kazi na serikali yoyote itakayoingia madarakani.
WEKA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment